Matukio 5 muhimu katika maisha ya kisiasa ya Merkel | NRS-Import | DW | 24.08.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

NRS-Import

Matukio 5 muhimu katika maisha ya kisiasa ya Merkel

Ujerumani inajiandaa kwa uchaguzi mkuu tarehe 24 mwezi ujao wa Septemba. Kansela wa sasa Angela Merkel anapania kushinda muhula wa nne madarakani.

Merkel, mtoto wa kike wa mchungaji aliyekulia enzi za utawala wa pazia la chuma, alianza kujishughulisha na siasa wakati upinzani dhidi ya serikali ulipoongezeka mnamo 1989, mwaka ambao ukuta wa Berlin ulianguka. Kwa kipindi kifupi alihudumu kama makamu msemaji wa serikali iliyochaguliwa kidemokrasia ya Ujerumani Mashariki, kabla kushinda uchaguzi mwaka 1990 na kuingia katika bunge la Ujerumani iliyoungana kama mwanachama wa chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union, CDU.

Aliyekuwa kansela wakati huo, Helmut Kohl, alimteua Merkel kama waziri wa masuala ya wanawake na vijana 1991, lakini akambatiza waziri wake huyo aliyekuwa na umri mdogo na jina la utani la "das Mädchen" yaani msichana mdogo.

Merkel alipanda ngazi katika uongozi wa chama cha CDU na kejeli za Kohl zilikuja kumgeukia wakati msichana Merkel alipokuwa mtu pekee aliyekuwa na ujasiri wa kumtaka ajiuzulu alipozongwa na kashfa ya rushwa ya kisiasa.

Merkel alichaguliwa mwenyekiti wa chama mwaka 2000 kwa kupata kura zaidi ya asilimia 95. Novemba 22 mwaka 2005, Merkel alikuwa kansela wa kwanza mwanamke na tangia hapo amefaulu kuchaguliwa mara mbili. Katika duru ya mwisho ya uchaguzi 2013, alikiongoza chama chake cha kihafidhina cha Christian Democratic Union, CDU, kupata matokeo bora kabisa katika uchaguzi tangu Ujerumani ilipoungana.

Merkel alipotangaza kuvifunga vinu vya nyuklia

Merkel aliushangaza ulimwengu alipotangaza kwamba vinu vya nyuklia vya Ujerumani vitafungwa kufikia mwaka 2022, kufuatia ajali mbaya katiak kinu cha nyuklia cha Fukushima nchini Japan mwaka 2011.

Ujerumani inaendelea kutumia viwanda vinavyoendeshwa kutumia nishati inayotokana na makaa ya mawe hadi pale itakapoimarisha miradi ya nishati isiyochafua mazingira. Nchi hii imewekeza sana katika nishati inayotokana na jua na upepo, na inalenga kutosheleza asilimia 80 ya mahitaji ya vyanzo vya nishati inayoweza kutumika tena na tena kufikia mwaka 2050.

Macho yote yalimgeukia Merkel wakati Ugiriki ilipotumbukia katika mgogoro wa deni mwaka 2010. Alitukanwa kama kiongozi mgumu asiye huruma, asiyetaka kutumia fedha. Pamoja na waziri wa fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble, alichukua msimamo mkali dhidi ya kuifutia deni serikali ya mjini Athens.

1608-19-DW-Wir-schaffen-das-Teaser-DEU.png

Bango kuhusu wahamiaji - Twayaweza haya

Akipewa jina la "Madame Non" katika maeneo ya Umoja wa Ulaya, Merkel hata hivyo alisonga mbele na kuunga mkono mikopo mitatu ya kimataifa ya thamani ya zaidi euro billioni 300 kuikoa Ugiriki isifilisike, lakini kwa masharti ya kubana matumizi na kuongeza kodi inayotozwa kwa kiwango kikubwa.

Merkel aliporuhusu wahamiaji kuingia Ujerumani

Merkel, ambaye anafahamika sana kama kiongozi makini na mwenye uangalifu mkubwa, alipata sifa katika ngazi ya kimataifa alipoifungua mipaka ya Ujerumani kwa wakimbizi wakati wa kilele cha mzozo wa uhamiaji barani Ulaya mwaka 2015, akiwashawishi Wajerumani na kauli mbiu - "Wir schaffen das" yaani Tunaweza.

Zaidi ya wahamiaji milioni moja wanaotafuta hifadhi, nusu wakitokea Syria, Iraq na Afghanistan, wamewasili Ujerumani tangu wakati huo, hivyo kuligawa taifa. Ingawa Merkel ametetea mara kwa mara uamuzi wake ulioibua utata, alisema haitajirudia tena wimbi kubwa la wahamiaji kuingia Ujerumani.

Wakati Donald Trump aliposhinda uchaguzi wa Mrekani mwaka 2016, Merkel alivunja utamaduni wa kutoa ujumbe wa kumpongeza huku akitoa mwito wa ushirikiano katika kuyalinda maadili ya demokrasia. Ujumbe huo ambao haukuwa wa kawaida ulivifanya vituo kadhaa vya habari kumtangaza kama kiongozi mpya wa ulimwengu huru, cheo ambacho Merkel alikipuuza, akisema inasikitisha kufikiri kwamba mtu mmoja na bila shaka sio kansela wa Ujerumani, kwamba angeweza kuyatatua matatizo ya ulimwengu.

Mipaka ya ushawishi wake ilijitokeza wakati wa mkutano wa kundi mataifa 20 yaliyoendelea zaidi kiuchumi na yanayoinukia kwa kasi kiuchumi, G20, ulioandaliwa na Ujerumani mwezi Julai mwaka 2017 mjini Hamburg, wakati viongozi waliposhindwa kupunguza tofauti zao na Trump kuhusu mabadiliko ya tabia nchi na ulinzi wa masoko.

Mwandishi: Josephat Charo/afpe

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com