Marekani yaziamrisha familia za wanadiplomasia wake kurudi nyumbani | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.07.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Marekani yaziamrisha familia za wanadiplomasia wake kurudi nyumbani

Serikali ya Marekani imeziamrisha familia za wanadiplomasia wa ubalozi wake wa Venezuela kurudi nyumbani na kutoa idhidi ya kuwaruhusu wafanyakazi wa ubalozi huo kuondoka kwa hiari, huku machafuko yakizidi kuwa mabaya.

Serikali ya Marekani hapo jana imeziamrisha familia za wafanyakazi wa ubalozi wake wa Venezuela kuondoka nchini humo, na wafanyakazi wa serikali kuondoka kwa hiari wakati wowote wanaoutaka, huku mgogoro wa kisiasa ukizidi kuwa mbaya, ikiwa ni siku chache kabla ya kufanyika uchaguzi wenye utata ambao wakosoaji wanasema utakuwa ndiyo mwanzo wa kutoweka kwa demokrasia katika taifa lenye utajiri wa mafuta.

Vifo vitano vimeripotiwa kufuatia vurugu za maandamano ya Alhamis, na kuifanya idadi jumla ya vifo katika miezi minne ya machafuko kufikia watu zaidi ya 100.

Wengi waliopoteza maisha katika maandamno hayo ya kuipinga serikali yaliyoanza mwezi Aprili ni vijana waliouwawa kwa kupigwa risasi. Idadi hiyo pia inajumuisha waporaji, polisi wanaodaiwa kushambuliwa na waandamanaji na raia wa kawaida waliouwawa katika ajali zilizotokana  na vizuwizi vilivyowekwa barabarani wakati wa maandamano hayo.

Mazungumzo ya amani na upinzani

Hapo jana akiwa anahutubia umati wa wafuasi wake, Rais wa Venezuela Nicolas Maduro amewataka raia wake kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa Jumapili ijayo uliogubikwa na utata, wa kuteua wajumbe wa baraza ambalo litapewa kibarua cha kuiandika tena katiba ya Venezuela.

Venezuela - Krise - Präsident Maduro (Reuters)

Rais wa Venezuela Nicolas maduro

Maduro pia alirudia tena pendekezo lake kwa upinzani la kukaa kitako pamoja kwa mazungumzo akidai kwamba ndio njia pekee ya kutatua mgogoro wa kisiasa uliolikumba taifa hilo.

"Ninapendekeza kwa upinzani wa Venezuela kuwa waachane na njia yao ya uasi, katika masaa machache yajayo, kabla ya uchaguzi wa kuteua Baraza la Taifa la Kuandika Katiba, tuanzishe mazungumzo, makubaliano ya kitaifa na maridhiano ya nchi yetu," amesema Maduro.

Upinzani umeitisha maandamanoo ya umma Ijumaa katika mji mkuu wa Caracas, jambo litakaloweza kuongeza kasi ya mvutano. Serikali kwa upande wake imepiga marufuku kufanyika maandamano yoyote kuanzia Ijumaa hadi Jumanne, baada ya kumalizika uchaguzi, hatua inayoweza kuongeza machafuko nchini humo.

Upinzani pia unawataka raia wa Venezuela kususia kura hiyo ya Jumapili, wakisema kwamba sheria za uchaguzi zina udanganyifu na zitahakikisha kuwa Maduro atapata wingi wa kura na kwamba katiba mpya itachukuwa nafasi ya demokrasia kupitia mfumo wa uongozi wa chama kimoja.

Vifo vilivyongezeka vya waandamanaji sasa vimekuwa chanzo kingine cha hasira miongoni mwa vijana wa Venezuela ambao huandamana mchana na kukusanyika nyakati za usiku na kupambana na maafisa wa polisi pamoja na walinzi wa taifa nchini kote.

Mapema wiki hii Marekani ilitangaza kuwawekea vikwazo viongozi 13 wa ngazi za juu wa Venezuela, wa sasa na wa zamani, kwa madai ya kuhusika na makosa ya rushwa, kudhoofisha demokrasia ya nchi na kushiriki katika vitendo vya ukandamizaji.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/ap

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com