1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSaudi Arabia

Marekani kuondoa marufuku ya uuzaji silaha kwa Saudi Arabia

26 Mei 2024

Marekani inatarajiwa kuondoa marufuku ya uuzaji wa silaha kwenda Saudi Arabia, gazeti la Uingereza la the Financial Times limeripoti.

https://p.dw.com/p/4gIUP
Ndege za kivita za Marekani
Ndege za kivita za MarekaniPicha: Mike Nelson/dpa/picture alliance

Gazeti la the Financial Times limeeleza kuwa marufuku hiyo huenda ikaondolewa katika muda wa wiki chache zijazo.

Financial Times, ikinukuu chanzo kinachofahamu suala hilo, imesema Marekani ilikuwa tayari imeieleza Saudi Arabia juu ya nia yake ya kuondoa marufuku hiyo.

Mara tu baada ya kuingia madarakani mnamo mwaka 2012, Rais Joe Biden alionekana kuchukua msimamo mkali juu ya kampeni ya Saudi Arabia dhidi ya kundi la wanamgambo wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran ambayo imesababisha vifo vya maelfu ya raia wasio na hatia nchini Yemen.

Soma pia: Jake Sullivan aelekea Saudi Arabia kujadili hali ya Mashariki ya Kati

Uhusiano kati ya Marekani na Saudi Arabia pia uliingia doa kuhusu rekodi mbaya ya haki za binadamu ya Riyadh hasa mauaji ya kinyama ya mwandishi na mkosoaji mkubwa wa utawala wa kifalme Jamal Khashoggi.

Saudi Arabia, mteja mkubwa zaidi wa silaha za Marekani, ilikasirishwa na vikwazo vya utawala wa Biden ikiwemo kusimamisha mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia licha ya tawala zilizopita za Marekani kuiuzia silaha nchi hiyo ya kifalme kwa miongo kadhaa.