1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaitaka Sudan kukata uhusiano na Korea Kaskazini

Iddi Ssessanga
1 Mei 2018

Afisa wa juu wa serikali ya Marekani amesema Sudan sharti ivunje uhusiano wote wa kibiashara na Korea Kaskazini kabla ya mazungumzo ya kuiondoa kwenye orodha ya ufadhili wa ugaidi. Sudan inasema haina uhusiano na Korea.

https://p.dw.com/p/2wxui
Sudan Präsident Omar Hassan al-Baschir
Picha: picture alliance/dpa/epa/P. Dhil

Marekani iliondoa vikwazo vya miongo kadhaa ilivyoiwekea Sudan mwezi Oktoba, lakini iliiacha kwenye orodha ya mataifa yanayofadhili ugaidi, jambo ambalo maafisa wa Sudan wanasema linazifanya benki za kimataifa kuhofia kufanya biashara na benki za Sudan, na hivyo kukwaza ufufukaji wa kiuchumi katika taifa hilo.

Maafisa wa Sudan wamekuwa wakishinikiza kuiondoa nchi hiyo kwenye orodha mbaya - ambayo inazijumlisha pia Korea Kaskazini, Syria na Iran -- wakati ambapo wanapambana na ongezeko la mfumuko wa bei, deni la taifa na upotevu wa mapato yatokanayo na mafuta.

Lakini Washington inasisitiza kwamba Khartoum itoe hakikisho kamili kwamba imevunja uhusiano na Pongyang, ambayo iliustua ulimwengu mwaka jana kwa kufanya majaribio kadhaa ya silaha za nyuklia na makombora ya masafa marefu.

Sudan Pressefreiheit Symbolbild
Raia wa Sudana akijisomea gazeti juu ya pikipiki yake. Sudan imekuwa ikikabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi hasa tangu ilipotengana na Sudan Kusini mwaka 2011.Picha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Marekani pia inaishinikiza Sudan kuboresha rekodi yake ya haki za binadamu, uhuru wa kuabudu na masuala mengine ya haki, ili kuyapeleka majadiliano na Khartoum kwa ngazi nyingine.

"Juu ya yote ni umuhimu wa kuvunja uhusiano wowote wa kibiashara na Korea Kaskazini," alisema afisa wa juu wa Marekani mwenye ufahamu kuhusu mazungumzo kati ya Washington na Khartoum, alipozungumza na shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotajwa jina.

"Kuna mengi tunayotaka kuona katika njia ya ushahidi tuliopatiwa kwamba biashara imesitisha." "Hakuna biashara zaidi, basi. Tupe ushahidi kwamba kwa uhakika unasitisha. Hilo ndiyo wanapaswa kufanya kwetu.

Sudan inasema haina uhusiano wowote na Pyongyang

Khartoum inasema imejifunga kuheshimu maazimio yote yaliopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini. "Sudan inathibitishakwamba haina uhusiano na Jamhuri ya Watu wa Korea kwa ngazi yoyote," ilisema wizara ya mambo ya nje ya Sudan kwenye taarifa siku ya Jumapili.

Wito huo kwa Sudan unakuja huku kukiwa na ishara za kuboreka kwa uhusiano kati ya Pyongyang na ulimwengu wa nje, ambapo kiongozi wa taifa hilo Kim Jong Un alikutana na mwenzake wa Korea Kusini Ijumaa wiki iliyopita, kuelekea mkutano wa kilele unaopangwa kati yake na rais Donald Trump.

USA Präsident Donald Trump Rede in Michigan
Utawala wa Trump uliiondolea Sudan vikwazo lakini ukaibakisha kwenye orodha mbaya ya mataifa yanayofadhili ugaidi.Picha: picture-alliance/AP Photo/P. M. Monsivais

Sudan na Korea Kusini hazina uhusiano wa kidiplomasia kwa miaka kadhaa, lakini baadhi ya mashirika ya haki za binadamu yanadai kwamba mataifa hayo mawili yana ushirikiano wa kijeshi.

Marekani iliweka vikwazo mwaka 1997 kuhusiana na madai kwamba Sudan inayaunga mkono makundi ya kijeshi. Mwasisi wa kundi la Al-Qaeda Osama bin Laden aliishi nchini Sudan kati ya 1992 na 1996.

Baada ya miaka kadhaa ya uhusiano mbaya baina yao, uhusiano kati ya Washington na Khartoum uliboreka chini ya utawala wa rais Barack Obama, na baadae ukapelekea kuondolewa kwa vikwazo na utawala wa Trump mwaka uliopita.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri: Mohammed Khelef