Marekani yafungia tovuti za habari za Iran | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.06.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Marekani yafungia tovuti za habari za Iran

Iran imeonya Jumatano (23.06.2021) kuwa hatua ya Marekani ya kufungia tovuti 33 zinazoendeshwa na vyombo vya habari vinavyohusishwa na Iran sio ya tija kwa mazungumzo ya nyuklia yanayoendelea .

Idara ya sheria  ya Marekani imesema mamlaka za nchi hiyo  imezifungia tovuti 33 za habari zinazothibitiwa na serikali ya Iran pamoja na tatu za kundi la Iraq la Kataeb Hezbollah ambazo imesema zilikuwa zinaendeshwa katika nchi yake kwa  kukiuka vikwazo. Tovuti hizo 33 zilikuwa zinamilikiwa na muungano wa redio na televisheni za kiislamu nchini Iran IRTVU unaodhibitiwa na kitengo cha jeshi la mapinduzi la iran kinachosimamia mapambano dhidi ya wapiganaji wa kikurdi IRGC.

Watumiaji  wa tovuti za habari zinazoongoza nchini Iran kama vile kituo cha televisheni cha Press na Al-Alam zinazopeperusha matangazo yao kwa lugha za kiingereza na kiarabu pamoja na kituo cha habari cha Al-Masirah kinachomilikiwa na kundi la Kihouthi la Yemen, walikutana na taarifa ya ukurasa mmoja iliyotangaza kufungiwa kwa tovuti hiyo na serikali ya Marekani na kufuatiwa na mihuri ya Ofisi ya Upelelezi ya Shirikisho na Idara ya Biashara ya Marekani. Zote IRTVU na IRGC zilikuwa zimewekwa katika orodha ya vikwazo vya Marekani na kufanya kuwa haramu kwa Wamarekani na kampuni za Marekani pamoja na kampuni za kigeni ama zisizokuwa za Marekani zilizo na matawi yake nchini Marekani kujihusisha nazo ama matawi yake.

Iran | Präsidentschaftswahlen

Ebrahim Raisi- Rais wa Iran

Shirika la habari la serikali ya Iran limeishtumu Marekani kwa kukandamiza uhuru wa kujieleza huku rais aliye mamlakani akihoji kuhusu wakati wa kuchukuliwa kwa hatua hiyo huku mazungumzo ya kuirejesha Marekani katika mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 kati yake na mataifa mengine yenye nguvu yakiendelea. Mkurugenzi wa ofisi ya rais Mahmoud Vaezi amewaambia wanahabari kwamba wanatumia njia zote za kimataifa na kisheria kulaani sera hiyo potovu ya Marekani.

Hatua hiyo ya Marekani pia inakuja baada ya kuchaguliwa kwa mhafidhina Ibrahim Raisi kama rais mpya wa Iran katika uchaguzi ambao wizara ya mambo ya nje ya Marekani umesema haukuwa huru na haki. Mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 uliifanya Iran kukubali kusitisha shughuli zake za nyuklia kwa kubadilishana na kulegezwa kwa vikwazo dhidi yake lakini mnamo mwaka 2018, aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump aliliondoa taifa hilo katika mktaba huo na kuongeza vikwazo dhidi ya Iran hali iliyochangia Iran kwenda kinyume na makubaliano ya awali ya kusitisha shughuli hizo za nyuklia.