Maoni ya wahariri | Magazetini | DW | 09.09.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Maoni ya wahariri

Wahariri wa magazeti leo wanavizungumzia vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi na juu ya hatari ya kufanyika mashambulio ya kigaidi nchini Ujerumani

Rais wa Urusi Wladimir Putin anyemelewa na vikwazo vingine

Rais wa Urusi Wladimir Putin anyemelewa na vikwazo vingine

Juu ya vikwazo zaidi dhidi ya Urusi gazeti la "Neue Osnabrücker" linasema Umoja wa Ulaya umejiingiza wenyewe katika mtego. Mhariri huyo anatilia maanani kwamba Umoja wa Ulaya unataka vikwazo vipya vieleweke kama njia ya kuishinikiza Urusi na siyo hatua ya uchokozi dhidi ya nchi hiyo.Mhariri huyo anasema siyo lazima mtu awe mrusi ili aweze kutambua kuwa hayo wanayoyasema mabalozi wa Umoja wa Ulaya ni kioja.

Hatari ya kutukia mashambulio ya kigaidi nchini Ujerumani

Gazeti la "Nordwest" linazungumzia juu ya hatari ya Waislamu wenye itikadi kali nchini Ujerumani wanaorejea kutoka nje wakiwa wamepikwa na wameiva itikadi za kigaidi. Lakini mhariri wa gazeti hilo anasema Ujerumani inajua namna ya kujihami dhidi ya magaidi hao. Gazeti hilo linaarifu kuwa Wajerumani watatu walikamatwa hapo jana walipowasili kutoka Kenya .Wametiwa mbaroni kutokana na kutuhumiwa kuwa magaidi.

Wanaitikadi kali wa kiislamu waliojipa kazi ya upolisi wa kuyalinda maadili ya uislamu katika bara bara za Ujerumani wamejiondoa kutoka kwenye barabara hizo baada ya polisi kuchukua hatua. Na yule mtu anaetuhumiwa kuwa mtegaji bomu amefikishwa mahakamani. Lakini pamoja na mafanikio hayo hailitakuwa shauri jema kufanya ajizi juu ya hatari ya ugaidi nchini Ujerumani.

Mhariri wa gazeti la "Nordwest" anatilia maanani kwamba tokea mwaka wa 2011 Wajerumani zaidi 400 wameenda Syria kupigana wanachokiita vita vya jihadi. Idadi kubwa ni vijana. Mhariri huyo anasema adhabu kali zinapaswa kutolewa pale sheria inapovunjwa, lakini la muhimu zaidi ni kuzing'oa mbegu za kasumba zinazoingia katika vichwa vya vijana hao.

Kura ya maoni Scotland

Watu wa Scotland sehemu iliyomo katika muungano na Uingereza, UK watapiga kura ya maoni kuamua iwapo wataendelea kuwamo katika muungano huo. Mhariri wa "Eisenacher Presse" anasema Waingereza sasa wanapiga vijembe.

Mhariri huyo anasema kwa Waingereza mjini London kusema ,watu wa Scotland watazama ikiwa watachagua kuwa huru, ni propaganda isiyokuwa na manufaa. Waingereza wangelianza mapema kufanya juhudi za kuwashawishi watu wa Scotland wabakie katika muungano. Sasa inabidi Waingereza wasubiri matokeo ya kura ya maoni na waone jinsi England na Scotland zitakavyohusiana katika siku za usoni.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Mohammed Adul-Rahman