1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Ushindi wa Macron fursa kwa Ulaya

Mohammed Khelef
25 Aprili 2022

Kuchaguliwa tena kwa Emmanuel Macron kuendelea na urais wa Ufaransa ni jibu pia la demokrasia ya Ulaya kwa mashambulizi ya Urusi na idhini ya kuendeleza ajenda ya kuliunganisha zaidi bara hilo, anasema Frank Hofmann.

https://p.dw.com/p/4AO1Z
Frankreich Präsidentschaftswahl Macrons Siegesfeier in Paris
Picha: Aurelien Meunier/Getty Images

Matokeo yako wazi kabisa: takribani asilimia 60 ya Wafaransa walimchaguwa tena Emmanuel Macron, lakini pia wakamuweka mgombea wa siasa kali za mrengo wa kulia kwenye nafasi yake kwa kumpa kiasi cha asilimia 40 ya kura.

Lakini Marie Le Pen anasalia na matakwa yake ya kuiondowa Ufaransa kutoka muungano wa kijeshi wa NATO na kuuvunja Umoja wa Ulaya.

Uchaguzi wa bunge utafanyika Juni. Na unapokuwa na mtu mmoja katika kila watatu aliyepigia kura upande wa siasa kali za mrengo wa kulia kwenye uchaguzi wa rais wiki mbili tu nyuma na takribani asilimia 20 ya waliokwenda kwa mgombea mwenye siasa kali za mrengo wa kushoto, Jean-Luc Melenchon, kitu kimoja kinakuwa wazi: nacho ni kwamba Wafaransa wanataka kubadilika kikamilifu. 

Mji mkuu Paris na tabaka lake la wanasiasa umejithibitishia usivyokuwa na umashuhuri kwengineko nchini Ufaransa. Zile hisia kwamba "wao wako juu huko na sisi tuko chini huku" zimejionesha wazi kwenye ukosoaji wa jinsi demokrasia yao ilivyofanya kazi. Na hili ni zaidi ya onyo.

Vuguvugu alilolianzisha Macron kwa jina linalomaanisha Jamhuri Kwenye Mwendo limebainisha nakisi ya demokrasia iliyopo kwa miaka mitano sasa, ambayo nayo pia imejibainisha kupitia kusambaratika kwa kambi za asili za kisiasa za wasoshalisti wa siasa kali na wahafidhina.

Macron na wenzake wanapaswa kulibadilisha hili ikiwa wanataka kuizuwia Ufaransa isiangukie kwenye siasa kali za kizalendo.

Ujumbe kwa Ulaya nzima

Na hilo linahusiana moja kwa moja na Ulaya nzima kwa ujumla wake, na juu ya yote, mshirika wake muhimu, Ujerumani.

Präsidentschaftswahl in Frankreich, Stichwahl, Marine Le Pen
Marie Le Pen.Picha: Francois Mori/AP Photo/picture alliance

Nchini Ufaransa, mara nyingi Umoja wa Ulaya unaonekana kama klabu ya kampuni kubwa na sio jumuiya ya kuwalinda ndani na nje.

Uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine ndani ya miezi miwili sasa umeonesha kwamba wengi wako sahihi kwenye hili.

Kwa kuwa vita vya Urusi ni pia mashambulizi dhidi ya Ulaya huru na ya kidemokrasia. 

Macron alichaguliwa miaka mitano iliyopita akiwa na ajenda ya wazi juu ya Ulaya – iliyoandikwa na Clement Beaune, ambaye sasa ni waziri wa masuala ya Umoja wa Ulaya katika wizara ya nje ya Ufaransa.

Kijana huyo wa miaka 40 aliandika kile kilichopaswa kufanywa na Macron, ambaye amemzidi kwa miaka minne tu: nacho ni kuiingiza Ufaransa zaidi kwenye Umoja wa Ulaya na kuugeuza Umoja huo kuwa wa kidemokrasia zaidi.

Lakini kufikia leo hakujawa hata na uamuzi wa wengi mjini Brussels juu ya masuala ya nje ya Umoja wa Ulaya.

Ni jambo la aibu kwamba rafiki wa Putin na waziri mkuu wa Hungray asiyeamini kwenye uliberali, Viktor Orban, anaweza kuzuwia maamuzi muhimu kwa kutumia veto.

Wakati Urusi inaishambulia demokrasia ya Ulaya kwa silaha, walipa kodi wa Ufaransa na Ujerumani wanalazimika kuendelea kumlisha adui mkubwa kabisa wa Ulaya nyumbani mwao.

Hili linaudhi.

Wafaransa wengi wamesema hivyo hivyo pia.

Macron ashinda awamu ya pili ya urais