Maoni: Somo kutoka Aleppo | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.12.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

VITA VYA ALEPPO

Maoni: Somo kutoka Aleppo

Kuangukia mji wa Aleppo mikononi mwa utawala wa Bashar al-Assad kunatuma ujumbe kuwa uhalifu wa kivita una ufaida na bila ya Urusi na Iran, basi Assad hawezi kupata ushindi wa kijeshi, anandika Rainer Sollich.

Spika wa bunge la Iran, Ali Laridzani, anasema kukombolewa kwa Aleppo kunamaanisha kuwa watu wa Syria wamefanikiwa dhidi ya magaidi. Lakini katika uhalisia, pongezi hizi ni ukosefu wa haya, maana ni kama kujipongeza mwenyewe.

Ushindi wa kijeshi wa utawala wa Assad kamwe usingeliwezekana kana si msaada mkubwa wa Iran na kundi la Kishia la Hizbullah la Lebanon, ambalo nalo linafadhiliwa na Iran. Kwa hakika, usingeliwezekana kabisa bila ya ushiriki wa moja kwa moja wa Urusi kwa mtindo wa mashambulizi yake ya kikatili ya anga kwenye maeneo yanayoshikiliwa na waasi na yale yanayokaliwa na raia.

Tangu hapo mwanzo na hadi sasa bado Aleppo inatwangwa kwa mabomu, wala hakuna upande wowote unaozingatia thamani ya uhai wa binaadamu. Kilichokuwa kinaangaliwa na ambacho hadi sasa kimo vichwani mwa waliomo kwenye vita hivi ni kumuangamiza adui tu, bila ya kujali madhara yatakayotokea.

Sollich Rainer Kommentarbild App

Na Rainer Sollich

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kumekuwa na mauaji ya maangamizi katika siku za hivi karibuni. Na hata baada ya washindi kuyatwaa majengo ya mwisho mwisho mikononi mwao, bado majanga zaidi yanahofiwa kutokea.

Bila Urusi na Iran, Assad hawezi kushinda kijeshi

Jambo moja lipo wazi: ushindi wa kijeshi wa utawala wa Assad hauzuiliki madhali tu anaendelea kutegemea washirika wake. Mara tu baada ya Aleppo yote kuwa mikononi mwake, sasa Assad ataelekeza mashambulizi yake kwenye jimbo la Idlib.

Kwa hivyo, vita vitaendelea na kuendelea kudai mihanga zaidi. Nani na nini kinaweza kumzuwia Assad?

Bila shaka, si mataifa ya Magharibi au hicho kiitwacho “jumuiya ya kimataifa!“ Umoja wa Mataifa umeshindwa moja kwa moja, kama alivyokiri Katibu Mkuu anayemaliza muda wake, Ban Ki-moon.

Dunia iliyashuhudia mauaji mjini Aleppo na maeneo mengine ya nchi hiyo bila kufanya lolote. Hata kama diplomasia ilikwenda hadi kwenye viwango vya juu kabisa, lakini ukweli ni kwamba ilikuwa diplomasia isiyo na maana: hakuna aliyejitokeza kuwasaidia raia wanaokandamizwa. Hili pia haliwezi kubadilishwa na rais ajaye wa Marekani, Donald Trump.

Kilicho wazi ni kimoja: kwamba uhalifu wa kivita una faida. Ndio ujumbe mchungu tunaoupata kutoka Aleppo. Na ujumbe mwengine ni kuwa hakuna kitakachokuwa nchini Syria, bila ya Urusi na Iran. Serikali za Iraq, Lebanon na Misri zinaweza kuwa zinaupendelea “mfumo mpya” unaokuwa sasa kwenye eneo lao.

Lakini Saudi Arabia na washirika wake wa Ghuba kamwe hawatalikubali hilo na hivyo kila upande utaendelea kutuma silaha kwa washirika wake. Hiyo maana yake ni kuwa mauaji yataendelea. 

Mwandishi: Rainer Sollich
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Grace Kabogo
 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com