1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya Uturuki na EU yanaweza kuimarishwa?

Angela Mdungu
4 Oktoba 2019

Ziara ya waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Uturuki na Ugiriki, inafanyika wakati hali katika kambi za wakimbizi zikizidi kuwa mbaya, na idadi ya wahamiaji wanaojaribu kuvuka mpaka kuelekea barani Ulaya ikiongezeka

https://p.dw.com/p/3QkAK
Türkei Beratungen zu Flüchtlingspakt in Ankara
Picha: picture-alliance/dpa/Turkish Foreign Ministry

Moto mkubwa uliozuka kwenye kambi yenye idadi kubwa ya watu ya Moria katika kisiwa cha Lesbos cha Ugiriki siku ya Jumapili, uliwakumbusha viongozi wa Ulaya juu ya hali ya kutisha inayowakabili wakimbizi. Kambi hiyo ilijengwa ikiwa na uwezo wa kuhifadhi watu 3,000 lakini kwa sasa ina  watu 12,000.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, ameambatana na Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa Christophe Castaner, pamoja na Kamishna wa uhamiaji wa Umoja wa Ulaya, Dimitris Avramopolous. Seehofer alisema, Ujerumani inataka kutoa msaada kwa Uturuki na Ugiriki.

Mkurugenzi wa taasisi ya kudumisha utulivu ya Ulaya, Gerald Knaus, anasema tukio la Lesbos lilikuwa linatabirika. Anasema maamuzi ya haraka ni muhimu katika kutatua mgogoro wa kiutu nchini Ugiriki. Knaus ameongeza kuwa, iwapo watu wakiachwa kwa miezi kadhaa katika mahali ambapo hawapati mahitaji, wala madaktari, mahali salama pa kuishi, na huduma za jamii majanga kama hayo yataendelea kutokea na kwamba makubaliano ya Umoja wa Ulaya na Uturuki ya mwaka 2016 yatakuwa hatarini.

Mtaalamu huyo wa masuala ya uhamiaji ambaye ndiye aliyechangia kuwepo makubaliano hayo, anakubali kuwa kwa mwaka uliopita, Ugiriki ilikuwa na idadi kubwa ya watu waliotuma maombi ya hifadhi katika Umoja wa Ulaya baada ya Cyprus.

Naye mwanachama wa upinzani wa chama cha mrengo wa kushoto wa Ujerumani Heike Hänsel ambaye husafiri mara kwa mara kwenda katika visiwa vya Ugiriki ameelezea mpango wa hivi sasa kama "sera ya kutenga", Ameongeza kuwa wakimbizi wanaishi visiwani humo katika hali zinazokiuka utu. Hensel amesema sera mpya ya uhamiaji inahitajika ndani ya Umoja wa Ulaya.

Ugiriki yatangaza kuimarisha mipaka

Siku ya Jumatatu, Ugiriki ilitangaza kuwa itaimarisha mipaka yake ya majini na nchi kavu, kufupisha mchakato wa kuomba hifadhi na kuwarejesha watu 10,000 wasiokidhi vigezo vya kupatiwa ulinzi mwishoni mwa mwaka ujao. Waziri wa uhamiaji wa Ugiriki Giorgos Koumoutsakos alisema, nchi yake inashughulikia takribani maombi 75,000 ya watu wanaotafuta hifadhi.

Die Lage der Flüchtlinge auf Lesbos
Baadhi ya wakimbizi wakiwa kwenye moja ya kambi katika kisiwa cha Lesbos, UgirikiPicha: DW/D. Tosidis

Mnamo mwezi Septemba, zaidi ya watu 10,000 wengi wao wakiwa familia kutoka Afghanistan na Syria walivuka Bahari ya Aegean kutoka Uturuki kuelekea Ugiriki. Kwa mujibu wa shirika la kuhudumia wakimbizi duniani UNHCR hiyo ni idadi kubwa zaidi katika kipindi cha miaka mitatu. 

Lengo kuu la mpango wa Umoja wa Ulaya na Uturuki la mwaka 2016 lilikuwa kuzuia wahamiaji kujaribu kuvuka kutoka Uturuki katika mazingra ya hatari na kupambana na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu.

Ingawa mpango huo ulifanikiwa kwa muda mfupi kabla ya kukwama, ongezeko la hivi sasa la idadi ya wakimbizi wanaoingia Ugiriki pamoja na vitisho vipya vya Rais wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan "kufungua mipaka" kunaleta wasiwasi kwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya hasa Ugiriki.