Mahakama ya juu Marekani yaruhusu marufuku ya kusafiri kuanza kutekelezwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.12.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mahakama ya juu Marekani yaruhusu marufuku ya kusafiri kuanza kutekelezwa

 Rais Donald Trump wa Marekani amepata ushindi baada ya majaji wa mahakama ya juu nchini humo kuamua amri ya marufuku yake dhidi ya wasafiri kutoka mataifa sita yaliyo na Waislamu wengi kuanza kutekelezwa

Hatua hiyo inafuatia mahakama ya juu nchini humo kubatilisha mapingamizi yaliyokuwa yamewekwa na mahakama za chini ambayo kwa kiasi fulani yalizuia utekelezaji wake.

 

Amri hiyo ilikua imewekewa pingamizi na wanasheria wa haki za binadamu kuwa ni marufuku dhidi ya Waislamu na kuwa inakiuka katiba ya Marekani na haikua na uthibitisho wa kutosha kuhusiana na hatari ya usalama kama ambavyo serikali imekua inadai.

Marufuku hiyo ya muda inayalenga mataifa ya Iran, Libya, Syria, Yemen, Somalia na Chad huku Korea Kaskazini na baadhi ya maafisa kutoka Venezuela wakiongezwa katika orodha ya sasa.

Trump bado ameendelea kusisitiza kua marufuku hiyo ni kwa ajili ya kulinda usalama wa Marekani.

Amri hiyo ya Trump ilikosolewa huku baadhi ya mahakama nchini Marekani zikiamua kuwa Trump hawezi kuwazuia walio na uhusiano na watu nchini Marekani kutoingia nchini humo.

Watu walioweka pingamizi dhidi ya amri hiyo walishawishi mahakama kusitisha utekelezaji wake wakati wao na wanasheria wa serikali wakitafuta uhalali kisheria kuhusiana na marufuku hiyo.

Hata hivyo, utawala wa Trump ambao unasema marufuku hiyo ni muhimu ili kuilinda Marekani na kuzuia mashambulizi ya kigaidi pamoja na usalama wa nchi hiyo kwa ujumla imepata uungwaji mkono mkubwa katika mahakama ya juu ambapo majaji saba dhidi ya wawili wameunga mkono marufuku hiyo iendelee wakati rufaa ikisubiriwa.

 Ikulu ya Marekani yasema haishangazwi na uamuzi wa mahakama

Taarifa ya ikulu ya Marekani-White House, imesema hawashangazwi na uamuzi wa mahakama ya juu wa kuruhusu mara moja kuendelea kwa utekelezaji wa marufuku hiyo ya rais inayolenga  nchi zinazohusishwa zaidi na masuala ya ugaidi.

Baraza linalohusika na masuala ya uhusiano  wa nchi za Kiislamu na Marekani ambalo ni shirika kubwa zaidi la kupigania haki za kiraia za waislamu limekosoa uamuzi huo wa sasa.

USA Proteste gegen Trumps neues Einreiseverbot (Getty Images/AFP/S. Huffaker)

Baadhi ya waandamanaji wakipinga marufuku hiyo ya kusafiri

Majaji wa mahakama ya juu wamesema wanatarajia mahakama za rufaa za chini kuharakisha uamuzi wao ili kutoa nafasi iwapo kutakua na uwezekano suala hilo kurejeshwa mahakama  ya juu likiwa ni pingamizi lingine la kisheria dhidi ya ikulu ya Marekani.

Mahakama ya San Francisco inatarajia kusikiliza kesi hiyo Jumatano na mahakama ya Richmond itafanya hivyo Ijumaa.

Trump alitangaza kwa mara ya kwanza  marufuku ya kusafiri baada ya kuingia rasmi madarakani  Januari mwaka huu. Hata hivyo baada ya  marufuku ya awali iliyohusisha mataifa sita muda wake kumalizika Septemba , utawala wa rais Donald Trump ulitangaza marufuku nyingine  na safari hii Chad ikiongezwa katika orodha wakati Sudan iliondolewa huku Korea Kaskazini na  Venezuela zikiongezwa pia.

Idara inayohusika na masuala ya uhamiaji pamoja na wanaharakati wanaopigania haki za kiraia wanasisitiza kwamba marufuku hiyo kimsingi bado inawalenga waislamu   na inakikuka  katiba ya Marekani kuhusiana na uhuru wa dini.

Mwandishi: Isaac Gamba/dw/afpe

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com