1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron: Hatufuti uwezekano wa kupeleka wanajeshi Ukraine

Bruce Amani
27 Februari 2024

Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema kuwa wanajeshi wake wanavizuia vikosi vya Ukraine kuvuka kutokea ukingo wa kulia wa mto Dnipro, karibu na kijiji cha Kynky katika jimbo la Kherrson nchini Ukraine

https://p.dw.com/p/4cvZh
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron Ukraine
Macron aliwaambia viongozi wa Ulaya kushirikiana kwa pamoja kuizuia Urusi kushinda vita UkrainePicha: Gonzalo Fuentes/AP Photo/picture alliance

Hayo ni wakati Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akisema kuwa hajafuta uwezekano wa kupelekwa wanajeshi wa nchi za Magharibi nchini Ukraine katika siku za usoni. 

Wakati vita vya Urusi nchini Ukraine vikingia mwaka wake wa tatu, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema hawezi kufuta uwezekano wa kupelekwa kwenye uwanja wa mapambano nchini Ukraine wanajeshi wa nchi za magharibi katika siku za usoni. Hii ni baada ya suala hilo kujadiliwa katika mkutano wa viongozi wa Ulaya mjini Paris hapo jana.

Mkutano wa usalama wa Ukraine katika Ikulu ya Elysee
Viongozi wa Ulaya wameonyesha mshikamano na UkrainePicha: Gonzalo Fuentes/AFP/Getty Images

Akizungumza katika Ikulu ya Elysee, kiongozi huyo wa Ufaransa alisema kila kitu kilijadiliwa kwa uwazi. "Hakuna maafikiano leo rasmi, ya uwazi, ya kuidhinisha kutuma askari wa ardhini. Lakini kwa suala la mienendo, hakuna kitu kinachopaswa kufutwa. Tutafanya kila linalohitajika kuhakikisha kwamba Urusi haiwezi kushinda vita hivi."

Mkutano huo uliwajumuisha zaidi ya wakuu 20 wa nchi na serikali za Ulaya na maafisa wengine wa Magharibi.

Macron alikataa kutoa maelezo kuhusu ni mataifa ambayo yanatafakari kuwapeleka askari wake, akisema anapendelea kuweko na kile alichokiita "utata wa kimkakati.”

Mkutano huo ulijumuisha Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani na Rais wa Poland Andrej Duda Pamoja na viongozi kutoka mataifa ya Baltic.

Marekani iliwakilishwa na mwanadiplomasia wake mkuu wa Ulaya James O'Brien, nayo Uingereza ikawalilishwa na Waziri wa Mambo ya Kigeni David Cameron.

Ujerumani: Hatutaiacha Ukraine kwenye vita peke yake

Duda alisema majadiliano kwa sehemu kubwa yalihusu kupelekwa wanajeshi nchini Ukraine na kukawa na makubaliano kuhusu suala hilo. Rais huyo wa Poland alisema anatumai katika siku za karibuni, wataweza kupeleka kwa Pamoja vifaa na silaha nchini Ukraine kwa sababu hicho ndio cha muhimu kwa sasa.

Macron alitaja haja ya kuimarisha usalama ili kukomesha mashambulizi yoyote ya Urusi dhidi ya nchi za ziada katika siku zijazo. Estonia, Lithuania na Latvia pamoja na Poland ambayo ni kubwa zaidi zinazingatiwa kuwa miongoni mwa nchi zinazoweza kulengwa katika upanuzi wa baadaye wa Urusi. Nchi zote nne ni washirika wakuu wa Ukraine.

Katika hotuba ya video, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine alitoa wito kwa viongozi hao waliokusanyika Paris "kuhakikisha kuwa Putin hatoweza kuharibu mafanikio yao na hatoweza kuutanua uvamizi wake kwa mataifa mengine.”

Zelensky amesema kuwa bila msaada mpya wa kijeshikutoka kwa Marekani, nchi yake haitaweza kuulinda ujia wa safari za meli katika Bahari Nyeusi ambao umewezesha Kyiv kusafirisha mamilioni ya tani za nafaka kwa masoko ya kimataifa.

afp, dpa