1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ligi ya mataifa ya Ulaya, makundi yapangwa

Sekione Kitojo
24 Januari 2018

Ujerumani wamepangwa pamoja na Ufaransa na Uholanzi katika ligi ya mataifa ya Ulaya ya UEFA ambayo inaanzishwa rasmi katika bara hilo, wakati mabingwa wa Ulaya, Ureno wakiwa katika kundi litakaloijumuisha Italia.

https://p.dw.com/p/2rRiJ
Nations League - Auslosung Trophäe
Picha: picture-alliance/dpa/J.-C. Bott

Kikosi  cha  kocha  Joachim Loew  cha  Ujerumani  kimo  katika  kundi  la  kwanza  la  ligi hiyo  ya  juu  kabisa , Ligi A, katika  tukio  la  kupanga  timu  lililofanyika  mjini  Lausanne nchini  Uswisi  leo  Jumatano (24.01.2018) kwa  ajili  ya  mashindano  hayo  mapya  ambayo kwa  kiasi  kikubwa  yatakuwa  badala  ya  michezo  ya  kirafiki.

Nations League - Auslosung Joachim Löw
Kocha wa Ujerumani Joachim Loew(katikati)Picha: picture-alliance/dpa/S. Di Nolfi

Ureno itakumbana  na  Italia  na  Poland katika  kundi  la  3  la  Ligi A wakati  Ubelgiji inapambana  na  Uswisi  na  Iceland  katika  kundi  la  2 , na  Uhispania  inakabana  na Uingereza  na  Croatia  katika  kundi la  4  katika  viwango  vya  juu vinne.

Michezo  itafanyika  kuanzia  Septemba  hadi Novemba  mwaka  huu  ambapo  bingwa  wa jumla  ataamuliwa  katika  michezo  ya  mchujo  ambayo  itwakutanisha  washindi  wanne  wa ligi  ya kundi A  Juni 2019.  Kila timu  katika  ligi  hizo nne  zitakuwa  na  michezo  ya  mchujo ili  kufikia  Euro 2020 kwa  ajili  ya  mshindi  wa  kundi, ama  timu ya  juu nyingine , ambae hatapata  nafasi  katika  fainali  kupitia michezo  ya mchujo.

Loew ameeleza  haja  ya  kukutana  na "timu vigogo"  kabla  ya  kupangwa  makundi  hayo na  huenda  akavunjika  moyo  kuona  kwamba  anakutana  na  timu  ngumu  kama  Ufaransa na  mahasimu  wao  wa  jadi  Uholanzi, wanaotarajia  kurejea  katika  hali  ya  kawaida baada  ya  kushindwa  kufuzu kucheza  katika  fainali  za  kombe  la  dunia  mwaka  2018 nchini Urusi.

Fußball Stars, deren Teams sich nicht für die WM qualifiziert haben | Robben Niederlande
Nahodha wa timu ya taifa ya Uholanzi Arjen RobbenPicha: imago/VI Images/M. van Steen

Ligi  ya  mataifa ya Ulaya 

Italia  pia  inatarajiwa  kupata  muda  wa  kujijenga  upya  baada  ya  kushindwa  kufikia katika fainali  za  kombe  la  dunia  nchini  Urusi  mwaka  huu, wakikosa  fainali  kwa  mara  ya kwanza  tangu  mwaka 1958.Uhispania  na  Uingereza  zinaonekana  kuwa  ni  timu  nyingine za  kiwango  cha  juu  lakini  mataifa  hayo  yote  katika  ligi A watatambua  kuwa , kwa kucheza  michezo  minne  tu , huenda  kutokea  matokeo  mabaya  na  kuteremshwa  kwa kumaliza  wakiwa  wa  mwisho katika  kundi  lao.

Watabadilishwa  na  washindi  wanne  wa  ligi B  ambayo  inajumuisha  Ireland ikikabana koo  na  Wales  na  Denmark katika  kundi  namba  4  na  Urusi , mara  baada  ya  kutoka katika  kuwa  mwenyeji  wa  kombe  la  dunia , inakumbana  na  Sweden  na  Uturuki  katika kundi  la  2.

Länderspiel Spieler Emre Can
Mshambuliaji wa Italia El - ShaarawyPicha: picture-alliance/augenklick/GES/M. Gilliar

Slovakia, Ukraine  na  Jamhuri  ya  Cheki  inafanya  kundi 1 wakati  kundi  la  3  lina  timu  za Austria , Bosnia-Herzegovina  na  Ireland  ya  kaskazini.

"Mara nyingi  tumepata  malalamiko  kwamba  timu  nzuri hucheza  na  timu  dhaifu , na  sasa watacheza  wenyewe," rais  wa  UEFA Aleksander Ceferin  alisema . "Wakati  huo  huo , timu dhaifu  sasa  zina  nafasi  kubwa  kufuzu  katika  mashindano  makubwa." Wakosoaji  hata hivyo , wamehoji  kama  kuna haja  ya  kuwa  na  mashindano.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae