Leo ni Siku ya Vijana Duniani | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.08.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Leo ni Siku ya Vijana Duniani

Maadhimisho hayo yanafanyika ulimwenguni kote ambapo kaulimbiu yake ni ''Majadiliano na Maelewano.''

default

Vijana wakipeperusha njiwa kama ishara ya kusherehekea siku yao.

Leo ni maadhimisho ya siku ya vijana duniani. Wakati siku hiyo inaadhimishwa ulimwenguni kote kwa njia mbalimbali, Umoja wa Mataifa nao umetangaza kuanza rasmi kwa mwaka wa vijana wa kimataifa hii leo. Siku hii ya vijana ambayo inaadhimishwa kwa njia mbalimbali katika kila taifa kaulimbiu yake ni ''Majadiliano na Maelewano.'' Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalojihusisha na masuala ya vijana, kaulimbiu hiyo itawasaidia vijana kutoka kila pembe ya dunia kutangaza amani kwa njia ya majadiliano miongoni mwao. Kwa upande wa mataifa ya Afrika Mashariki, siku hii inaadhimishwa na vijana kwa kufanya msafara wa amani ulioanza jana mjini Arusha, Tanzania na ambao utamalizikia nchini Burundi, Agosti 18, mwaka huu. Vijana hao watabadilishana mawazo na kufundishana juu ya umuhimu wa amani kwa nchi za Afrika Mashariki. Aidha, wakati leo vijana wanaadhimisha siku yao, Umoja wa Mataifa nao umetangaza kuanza rasmi kwa mwaka wa vijana wa kimataifa hii leo. Mwaka huo umetangazwa kwa kuzingatia azimio la kimataifa kifungu A/RES/64/134. Uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano mkuu wa Baraza la Umoja wa Mataifa mwaka 2009.

Wakati vijana leo wakiadhimisha siku yao, Shirika la Kazi Duniani-ILO limesema kuwa idadi ya vijana duniani wasio na ajira imefikia milioni 81.2, kwa mwaka uliopita. Shirika hilo limesema kuwa kiwango cha vijana wasio na ajira duniani kimekua mara mbili zaidi kuliko kwa watu wazima kwa asilimia 1.1 katika kipindi cha miaka miwili, hivyo kuathiri asilimia 13 ya vijana wenye kati ya umri wa miaka kuanzia 15 hadi 24. Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Juan Somaiva amesema kuwa vijana ni watu wanaoongoza maendeleo ya kiuchumi. Kwa mujibu wa shirika hilo, karibu vijana milioni 73 walikuwa hawana ajira mwaka 2007. Ripoti ya Shirika hilo la Kazi Duniani imeeleza kuwa kitendo cha vijana kukosa ajira kinawasababisha vijana hao kujiingiza katika makundi maovu kutokana na kukaa bure bila kuwa na shughuli ya kufanya, hivyo kujihusisha na uhalifu. Aidha, ripoti hiyo imesema ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana pia huwafanya vijana hao kupata matatizo ya kiakili, kujihusisha na ghasia na matumizi ya dawa za kulevya.

Shirika hilo limesema kuwa maeneo yenye idadi kubwa ya vijana wasio na ajira ni katika mataifa yanayoendelea kiuchumi. ILO imebainisha kuwa hata katika mataifa yaliyoendelea kama vile Marekani, mataifa ya Umoja wa Ulaya na mataifa yaliyokuwa ya kikomunisti ambayo yako nje ya Umoja wa Ulaya, nayo pia yanaanza kuona kwamba kuna ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana. Kati ya mwaka 2008 na 2009, kiwango cha vijana wasiokuwa na ajira wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 24 katika mataifa yaliyoendelea kiuchumi, kilipanda na kufikia asilimia 4.6, ambapo kwa dunia nzima kwa ujumla kilifikia asilimia 17.7. Hata hivyo, Bwana Somaiva amezitolea wito serikali za mataifa yote tajiri na masikini kuhakikisha yanalenga kutoa elimu bora na mafunzo ili kukabiliana na tatizo hilo. Mkuu huyo wa ILO pia amezitaka serikali hizo kuongeza ajira miongoni mwa vijana kwani wao ndio nguvu kazi ya taifa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (Un.org.youth,AFPE,RTRE)

Mhariri:Josephat Charo

 • Tarehe 12.08.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ojft
 • Tarehe 12.08.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ojft
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com