1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kwa nini Umoja wa Ulaya hauna ushawishi Mashariki ya Kati?

Mohammed Khelef
19 Mei 2021

Licha ya Umoja wa Ulaya kuwa mfadhili na muungaji mkono wa pande mbili za mgogoro mkongwe wa Mashariki ya Kati, ukweli ni kuwa si Jerusalem wala Gaza wanasubiri kauli za watu wa Ulaya kuutatuwa mzozo huo.

https://p.dw.com/p/3tb2C
Informeller EU-Sozialgipfel in Portugal | Ursula von der Leyen
Picha: Tiago Petinga/REUTERS

Kwa takribani miaka 25 sasa, Umoja wa Ulaya umekuwa ukiisaidia kifedha serikali ya Palestina, miradi ya maendeleo na elimu kwenye maeneo ya Ukanda wa Gaza, Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki. 

Wenyewe Umoja huo unasema kwamba hutumia fedha nyingi zaidi kwa Wapalestina kuliko kwengine kokote katika Mashariki ya Kati.

Baina ya mwaka 2017 na 2020, mataifa ya Umoja wa Ulaya peke yao yalichangia jumla ya euro bilioni 2.3 kama msaada wa moja kwa moja kwa Palestina. 

Kwa miaka mingi sasa, Umoja wa Ulaya umekuwa ukitowa msaada wa kijamii kwa zaidi ya watu 100,000 katika Ukanda wa Gaza, eneo linalotawaliwa na Hamas, ambalo kwa mujibu wa Umoja huo ni la kigaidi.

Umoja wa Ulaya pia unalipia sehemu ya mishahara na gharama za kiutawala za serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina yenye makao yake katika Ukingo wa Magharibi. 

Haitoshi, kila mwaka euro milioni 159 hutolewa kwenye bajeti ya Umoja huo kwenda Shirika la la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina (UNWRA).

Kando ya fedha hizo, Ujerumani peke yake inachangia euro milioni 210 kwenye bajeti ya UNWRA.

Mfadhili asiye na nguvu za kisiasa 

Israel - Palästina-Konflikt
Mwanajeshi wa Israel akitayarisha makombora karibu na mpaka wa Israel na Gaza siku ya tarehe 18 Mei 2021.Picha: Baz Ratner/REUTERS

Wakati huu ambapo Israel na kundi la Hamas wako kwenye mapigano, ilitazamiwa kwamba angalau Umoja wa Ulaya ungelikuwa na ushawishi wa kushinikiza usitishaji mapigano ambao unasema inataka kuuona na pia wenyewe kuwa sehemu muhimu ya upatanishi. 

Lakini mchambuzi wa masuala ya Mashariki ya Kati katika Taasisi ya Sera za Ulaya mjini Brussels, Mihai Sebastian Chihaia, anasema ndani ya Umoja wa Ulaya kuna mpasuko linapohusika suala la Mashariki ya Kati, kwa kuwa na mataifa yanayoelemea Israel kama ilivyo Ujerumani na yanayoelemea Palestina kama ilivyo Sweden.

"Umoja wa Ulaya ina nyenzo zote muhimu za kuanzisha mkakati wa kusonga mbele kwenye eneo la Mashariki ya Kati. Lakini inahitaji dhamira ya kisiasa kuutekeleza mkakati huu. Dhamira hii ya kisiasa ndiyo ambayo imekosekana," anasema Chihaia.

Kisiasa, Umoja wa Ulaya unaendelea kung'ang'ania suluhisho la madola mawili huru yanayoishi kwa usalama baina yao: la Israel na la Palestina.  

Lakini ili kulifikia suluhisho hilo, ambalo muda wote linazungumzwa bila kutekelezwa, kunahitajika usimamizi usioelemea upande wowote. Na huo, wachambuzi wengi wanaona, ni shida kupatikana ndani ya Umoja wa Ulaya.