1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Mwanamke wa Zimbawe akiwa na mtoto wake huku akimvuta Punda.Picha: PA/dpa

Kushuka kwa uchumi Zimbabwe kwa walazimu wanawake kujiuza wapate chakula.

Scholastica Mazula
23 Mei 2008

Wanawake nchini Zimbabwe wamekuwa wakilazimika kuuza miili yao kwa ajili ya kujipatia chakula nchini Msumbiji.

https://p.dw.com/p/E52p

Hali hii inafuatia kushuka kwa Uchumi nchini Zimbabwe kitendo kinachowafanya raia wake kutafuta njia mbalimbali za kuweza kumudu maisha.

Nyasha ni mama mwenye watoto wawili ambaye amekuwa akihangaika kutafuta chakula kwa ajili ya familia yake, amereje nyumbani kwake nchini Zimbabwe baada ya kufanya kazi ya ukahaba katika nchi jirani ya Msumbiji kutokana na kuambiwa kuwa ndiyo njia pekee ya kuweza kujipatia dola.

Mama huyo mwenye umri wa miaka ishirini na tatu aliyeko katika Mji wa Chimoio nchini Msumbiji, anasema anapata kiasi kidogo sana cha fedha lakini endapo atakitunza vizuri ataweza kutuma fedha kidogo nyumbani ili ziweze kuisaidia familia yake.

Nyasha anasisitiza kuwa ni vigumu sana kurejea nchini Zimbabwe na kupata kazi na nchini Msumbiji hawawezi kupata kwa sababu hawana vibali maalumu vya kuishi na ndiyo sababu kubwa inayowafanya wanawake wengi kufanya biashara ya ukahaba.

Kuanguka kwa uchumi nchini Zimbabwe kumewafanya raia wengi wa nchi hiyo kukimbilia nchi jirani kwa ajili ya kutafuta maisha bora, lakini hoteli nyingi za mitaani katika mpaka wa Zimbabwe na Msumbiji zimekuwa zikishuhudiwa kuwepo kwa wahamiaji wengi wa kike.

Hoteli moja ya Madrinha iliyoko mjini Chimoio, zamani ilikuwa moja ya hoteli za bei nafuu lakini yenye kuheshimika kwa ajili ya wasafiri.Lakini hivi sasa imejaa wanawake raia wa Zimbabwe ambao wanasifika kwa kujiuza kwa bei nafuu.

Nyasha anasimulia kuwa alisikia kutoka kwa marafiki zake kwamba biashara ya ukahaba inafaida sana nchini Msumbiji ambayo inaweza kukuingizia dola za kutosha, lakini ameamua kurejea nchini mwake kwa sababu hajapata kiasi chochote cha dola.

Chimoio iko kilomita miambili kutoka mpakani na Zimbabwe na nikituo kikubwa cha madereva wanaosafiri kwenda nchi jirani za Malawi, na Zambia kupitia bandari ya Msumbiji ya Beira.

Afisa wa ngazi za juu wa Asasi isiyo ya Kiserikali inayojishughulisha na masuala ya Kiafya, Faruk Aboobakar, anasema ongezeko la ukahaba limeanza kuzitia wasiwasi taasisi nyingi zilizoko kwenye sector inayoshughulikia masuala ya afya ya kijinsia.

Afisa huyo anasema hili ni tatizo kubwa sana, akizingatia tatizo la wanawake wengi wa Zimababwe kujihusisha na biashara ya Ukahaba.Lakini anasema kwa bahati nzuri utafiti unaonyesha kuwa wanawake wengi wanasisitiza matumizi ya Kondomu wakati wakifanya biashara hiyo.

Julia Afredo, ni mama mwenye umri wa miaka ishirini na tano akiwa na watoto watatu na anaishi karibu na Hoteli ya Mdrinha, anasema anasikitishwa sana na hali hiyo na anahofia pia mtoto wake wa kike asije akaathirika na hali hiyo.

Anasema wasiwasi wake ni juu ya watoto wake wasije wakafikiri kwamba huwenda kila mwanamke wa Zimbabwe anafanya biashara ya Ukahaba.

Bibi Julia anasema wanatambua kuwa wanawake hao wanamatatizo nchini mwao, lakini kitendo cha kuuza mwili hakiwasaidii na wala siyo suluhisho la matatizo ya maisha yao na kwamba wanapaswa kutafuta njia nyingine za kujiingizia kipato.

Nchini Zimbabwe biashara ya Ukahaba hairuhusiwi na mwanamke yeyote atakayeonekana kuifanya hukamatwa tofauti na nchini Msumbiji sheria haiichukulii biashara hiyo kama kosa la jinai.

Uchumi wa Zimbabwe imeshuka katika kipindi cha muongo mmoja uliopita na kusababisha kupanda kwa gharama ya maisha kufikia asilimia mia moja sitini na tano na asilimia themanini ya watu wake hawana ajira.