Korea Kaskazini yajaribu makombora mapya ya masafa marefu | Matukio ya Kisiasa | DW | 13.09.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Korea Kaskazini yajaribu makombora mapya ya masafa marefu

Korea Kaskazini imesema imefanikiwa kufanya majaribio ya makombora mapya ya masafa marefu mwishoni mwa wiki iliyopita. Haya ndiyo majaribio ya kwanza kufanywa na taifa hilo katika kipindi cha miezi kadhaa.

Majaribio haya yanaonyesha jinsi nchi hiyo inavyozidi kupanua uwezo wake wa kijeshi wakati ambapo kuna mkwamo wa majadiliano ya nyuklia kati yake na Marekani.

Kituo kikuu cha habari cha Korea Kaszini KCNA kimesema Jumatatu kuwa, makombora hayo ambayo yalikuwa yanaundwa kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita, yamekwenda umbali wa kilomita 1,500 wakati wa majaribio hayo hapo Jumapili na Jumamosi.

Jeshi la Korea Kusini halikuthibitisha moja kwa moja

Nchi hiyo imeyasifu makombora hayo ikisema ni zana zenye umuhimu mkubwa ambazo zinaafiki wito wa kiongozi Kim Jong Un wa kuliongezea nguvu jeshi la nchi hiyo. Kim hakuwepo katika majaribio hayo huku kituo cha habari cha KCNA kikisema mwanachama wa chama tawala cha Wafanyakazi ambaye pia ni katibu wa kamati yake kuu Pak Jong Chon ndiye aliyehudhuria.

Nordkorea | Militärparade in Pyongyang

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un

Jeshi la Korea Kusini halikuthibitisha moja kwa moja majaribio hayo ingawa limesema linachunguza kupitia kitengo chake cha ujasusi. Boo Seung-chan ni msemaji wa jeshi la Korea Kusini.

"Kulikuwa na swali la iwapo tulifahamishwa na jeshi la Korea Kaskazini kuhusiana na majaribio hayo au iwapo kulikuwa na ujumbe wowote kupitia jeshi. Nitalijibu hivi swali hilo, njia ya mawasiliano ya Kusini na Kaskazini haifanyi kazi," alisema Chan.

Marekani nayo kupitia wizara yake ya ulinzi imetoa tamko na kusema majaribio hayo ya makombora ni kitisho kwa nchi jirani na jamii ya kimataifa. Imezidi kusema kuwa inaendelea kuitazama hali jinsi ilivyo na inashauriana kwa karibu na nchi marafiki na washirika.

Korea Kaskazini ina vikwazo vya kimataifa

Marekani imesema inaendelea na dhamira yake ya kuwalinda majirani wa Korea Kaskazini Japan na Korea Kusini. Korea Kusini na Marekani wako katika makubaliano ambapo karibu wanajeshi 28,500 wa Marekani wako Korea Kusini ili kuilinda nchi hiyo dhidi ya jirani yake aliyefanya uvamizi mwaka 1950.

Tazama vidio 01:03

Korea Kaskazini yafyatua tena makombora

Korea Kaskazini imewekewa vikwazo vya kimataifa vya silaha zake za nyuklia na mpango wake wa makombora ya masafa marefu. Taifa hilo linasema linahitaji silaha hizo ili kujilinda kutokana na uvamizi wa Marekani.

Lakini wachambuzi wanasema, kujihami huku kwa Korea Kaskazini na silaha za nyuklia na makombora ya masafa marefu ni njia ya kuweka wazi matakwa yake ya kisiasa kwa Marekani na Korea Kusini. Korea Kaskazini inajaribu kuuwekea shinikizo utawala wa Rais Joe Biden, kuhusiana na kuiondolea vikwazo vya kidiplomasia baada ya Kim Jong Un kukataa kuharibu silaha zake kwa ajili ya manufaa ya kiuchumi wakati wa utawala wa Donald Trump.

Vyanzo: AFPE/Reuters/AP