1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kizazi cha mwisho waitisha maandamano miji 10 Ujerumani

Iddi Ssessanga
11 Machi 2024

Kundi la wanaharakati wa mazingira la Last Generation, au "Kizazi cha Mwisho" limewataka watu kujiunga na aina mpya ya maandamano katika miji 10 ya Ujerumani wakati wakianzisha awamu mpya ya maandamano.

https://p.dw.com/p/4dP6I
Ujerumani | Maandamano ya Tabianchi| Last Generation mjini Berlin
Wanaharakati wa Kizazi cha Mwisho wakifanya mzingiro wa amani wa mtaa mjini Berlin, Ujerumani, Novemba 25, 2023.Picha: Nadja Wohlleben/REUTERS

Kundi la wanaharakati wa mazingira la Last Generation limetoa wito kwa watu kujiunga na aina mpya ya maandamano katika miji 10 ya Ujerumani siku ya Jumamosi, ili kuanza msimu wa maandamano.

"Mabaraza ya ukaidi " yamepangwa katika miji ya Berlin, Bremen, Cologne, Leipzig, Karlsruhe, Freiburg, Stuttgart, Regensburg, Munich na Rügen, kundi hilo lilisema siku ya Jumatatu.

Kundi hilo limesema maandamano mapya yatachukua muundo wa umati wa watu wanaofunga barabara na njia za waendao kwa miguu. Mikutani hii inapaswa kuwa "ya kutotii zaidi" kuliko maandamano ya kupangwa, lakini "ya amani kabisa," lilisema kundi hilo.

Soma pia:Michango ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kupungua kabla ya mkutano wa COP28

Haikuwa wazi hasa jinsi mikusanyiko inapaswa kuonekana na muda gani ingedumu. Kundi hilo lilianza kuandamana kwa kuziba mitaa zaidi ya miaka miwili iliyopita ili kuvutia nadhari kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kudai hatua za kukabiliana nayo.

Hapo awali, wanaharakati walijibandika kwenye barabara kuu ili polisi wasiweze kuwaondoa kwa urahisi.

Ujerumani | Maandamano ya Last Generation mjini Berlin
Wandamanaji wa Last Generation wakiwa nyuma ya bango lao lenye maneno ya KIjerumani yenye tafsiiri ya "Madiliko ya Tabianchi."Picha: Nadja Wohlleben/REUTERS

Lakini Last Generation ilisema mwezi Januari kwamba wanachama hawatajigandisha tena kwenye sakafu za barabara - mbinu ya usumbufu ambayo ilivuta hisia kwa hoja zao hata kama ilisababisha hasira za madereva, wasafiri wa ndege na polisi.

Pia walifanya maandamano katika majumba ya makumbusho, viwanja vya michezo na wizara. Polisi ya Berlin pekee ilihesabu maandamano 550 mwaka jana.

Soma pia:Vijana waandamana kabla ya mkutano wa mabadiliko ya tabianchi 

Lakini wanaharakati wengi wamekabiliwa na kesi na ofisi ya mwendesha mashtaka mjini Neuruppin inalichunguza kundi hilo kwa tuhuma za kuunda shirika la uhalifu.

Kundi hilo pia lilimtaka Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier kushughulikia mzozo wa tabianchi katika hotuba yake kwa taifa na kuanzisha mjadala juu ya hatua za haraka, ikiwa ni pamoja na kuondolewa mara moja kwa nishati zote za mafuta.

Wanaharakati wa mazingira wakizuwia mtaa.
Waandamanaji wa Last Generation walikuwa wanatumia mbinu ya kujigandisha barabarani na kuzuwia usafiri, huku polisi wakitumia nguvu na mbinu za ziada kuwabandua.Picha: Andreas Stroh/ZUMA/picture alliance

Kundi hilo pia lilidai ushuru wa mali ili kufadhili ulinzi wa hali ya hewa na "mgao wa haki ambao unaweka kikomo juu ya matumizi ya kupita kiasi ya matajiri," katika mkutano na waandishi wa habari karibu na makazi yake rasmi mjini Berlin.

Chanzo: DPA