1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa zamani wa Proud Boys afungwa miaka 22 jela

Josephat Charo
6 Septemba 2023

Kiongozi wa zamani wa kundi la Proud Boys Enrique Tarrio amehukumiwa miaka 22 gerezani kwa ushiriki wake katika shambulizi dhidi ya bunge la Marekani Januari 6 mwaka 2021.

https://p.dw.com/p/4VzcY
USA I Enrique Tarrio I Proud Boys
Picha: Allison Dinner/AA/picture alliance

Kiongozi wa zamani wa kundi la waasi wa kizalendo la Proud Boys Enrique Tarrio amehukumiwa kifungo cha miaka 22 jela kwa jukumu lake katika shambulizi dhidi ya bunge la Marekani mnamo Januari 6 mwaka 2021. Jaji Timothy Kelly amesema wakati wa kusikilizwa kwa hukumu kulikodumu takriban saa nne mjini Washington kwamba siku ya uvamizi huo ulivunja utamaduni ambao ulikuwa haujawahi kuvunjwa hapo awali wa kuhamisha madaraka kwa amani.

Hukumu hiyo inaelezwa kuwa kali na ya kipindi kirefu kabisa kuwahi kutolewa kufikia sasa kuhusu uvamizi huo. Waendesha mashtaka walitaka Tarrio afungwe miaka 33 jela. Tarrio hakuwepo mjini Washington siku ya uvamizi lakini alituhumiwa kwa kuelekeza shambulizi hilo lililofanana na la kijeshi kufanywa na wanachama wa kundi la Proud Boys.

Tarrio mwenye umri wa miaka 39 na wanachama wengine kadhaa wa Proud Boys walipatikana na hatia ya kula njama za uchochezi mwezi Mei kwa majukumu yao katika jaribio la kusimamisha uidhinishaji wa bunge wa ushindi wa mgombea wa chama cha Democratic rais wa sasa Joe Biden wa 2020 dhidi ya rais wa zamani Donald Trump.

Mwanachama mwingine wa kundi hilo Ethan Nordean alihukumiwa kifungo cha miaka 18 jela na jaji Kelly wiki iliyopita.