1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Kamati ya Jan. 6: Trump aliwasha 'moto' wa uasi Capitol Hill

Iddi Ssessanga
23 Desemba 2022

Kamati ya Bunge ya Januari 6 imetoa ripoti yake ya mwisho kuhusu shambulizi "lisilofirikika" dhidi ya Capitol, na wafuasi wa rais Donald Trump, na kulitikisa taifa hilo na kudhihirisha udhaifu wa demokrasia ya Marekani.

https://p.dw.com/p/4LMLx
USA Untersuchung des Capitol Riot
Picha: J. Scott Applewhite/AP Photo/picture alliance

Ripoti hiyo yenye kurasa 814 inatoa maelezo ya kuvutia kuhusu juhudi za mwezi mzima za Trump kubatilisha uchaguzi wa rais wa mwaka 2020, na inataja mapendekezo 11 kwa bunge la Congress na watendaji wengine kuzingatia ili kuimarisha taasisi za taifa hilo dhidi ya majaribio yoyote ya baadae kuchochea uasi.

Pamoja na ripoti hiyo, kamati hiyo inatoa pia nakala kadhaa za maelezo ya mashahidi kutokana mahojiano yake zaidi ya 1,000 na maelezo mapya ya kushangaza. Wiki hii, ilipendekeza Rais huyo wa zamani afunguliwe mashtaka ya uhalifu. Mwenyekit wa kamati hiyo Bennie Thompson, alisema katika dibaji ya ripoti hiyo kuna maswali mengi yanayosalia.

"Uongo mkubwa"

Kwa Rais wa Marekani kuchochea kundi la wafanya fujo kuvamia bunge na kuzuwia kazi ya Congress siyo hali ambayo taasisi zetu za intelijensia na usimamizi wa sheria zilitaraji kwa nchi hii, alisema Thomson, Mdemokrat anaewakilisha jimbo la Mississipi, na kuongeza kuwa kabla ya Januari 6, hilo lilikuwa jambo lisilofikirika.

USA Untersuchung des Capitol Riot
Kurasa za muhtasari wa ripoti kuhusu mashambulizi ya Januari 6, 2021 dhidi ya jengo la bunge la Congress zilipigwa picha Desemba 19, 2022 mjini Washington.Picha: Jon Elswick/AP Photo/picture alliance

Kuanzia kile kilichoitwa "Uongo Mkubwa" wa madai ya Trump katika usiku wa siku ya uchaguzi wa Novemba 2020 kuhusu uchaguzi ulioibwa hadi mzingiro wa bunge Januari 6, 2021, ripoti hiyo inataja mwanzo na mwisho wa uvamizi huo ulioshuhudiwa kote duniani.

Soma pia: Trump atangaza kuwania urais 2024

Inafafanua jinsi Trump na wafuasi wake walivyoshiriki katika mpango mpana wa kutengua ushindi wa Joe Biden katika uchaguzi wa rais - kwanza kupitia pingamizi za mahakamani, kisha, baada ya kushindwa kwa mbinu hizo, kwa kuandaa wajumbe wa majimbo kupinga ushindi wa Biden.

Kushindwa kuwazuwia wafanya fujo

Wakati Bunge likijiandaa kukutana kuhakiki matokeo ya uchaguzi, Trump aliita kundi la wafanya vurugu mjini Washington kuhudhuria mkutano wa "Zuwia Wizi" katika viwanja vya Ikulu ya White House.

Baada ya mikutano kadhaa ya hadhara, ripoti hiyo pamoja na nyaraka nyingine zinazoandamana nayo, zinatoa maelezo zaidi ya kina kuhusu vipengele muhimu vya mipango ya timu ya Trump kubatilisha uchaguzi, kujiunga na kundi la wafanya vurugu kwenye eneo la Capitol, na, baada ya kamati kuanza uchunguzi, kuwatia kishindo wale ambao wangetoa ushahidi dhidi yao.

Soma pia: Mashahidi: Trump alitaka kujiunga na vurugu za Capitol Hill

Ripoti hiyo pia inaeleza kushindwa kwa Trump kuchukua hatua zozote wakati wafuasi wake walikuwa wakivamia jengo la bunge la vurugu.

Viongozi duniani walaumu uvamizi wa majengo ya bunge na seneti nchini Marekani

Trump amejaribu kuishushia hadhi ripoti hiyo, kwa kuwashambulia wajumbe wa kamati na kuwataja kama 'majambazi na walaghai' huku akiendelea kupinga bila uthibitisho kushindwa kwake mwaka 2020. Akizungumzia hatua ya kamati kupendekesha afunguliwe mashtaka, Trump alisema wajumbe hao hawaelewi maana kila wanapomuandama, watu wanaopenda uhuru wanazidi kuungana naye, na kwamba hatua hiyo inamuimarisha tu.

Chanzo: Mashirika