Kashfa ya Marekani kutega mawasiliano kuathiri uchumi
3 Julai 2013Wanasiasa wa Ujerumani wameonesha hasira zao kwa kile kinachoonekana kama kiwango kikubwa kabisa cha taarifa ambazo Marekani huzikusanya kutoka nchi hii kupitia utegaji wa mawasiliano ya simu na mitandao. Kiasi cha taarifa nusu bilioni hukusanywa kila mwezi.
Lakini licha ya kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka, jambo ambalo haliwezi kusahaulika ni kwamba Ujerumani, Umoja wa Ulaya na Marekani ni marafiki wakubwa.
Hapo jana Ujerumani ilikataa maombi ya hifadhi yaliyotumwa na Edward Snowden, mtu aliyevujisha taarifa kadhaa za kijasusi ikiwemo hii ya Marekani kuwachunguza washirika wake wa jadi, licha ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, kukiri kwamba kupokea maombi hayo.
“Ninaweza kuthibitihsa kwamba leo majira ya asubuhi kiasi cha saa 8 na dakika 11 tumepokea maombi ya hifadhi ya Bwana Snowden. Sasa tutayapitia maombi haya kwa haki na kwa sheria.“ Alisema Westewelle.
Ulaya haiko tayari kukwaruzana na Marekani
Kuonesha kwamba hakuna nchi ya Ulaya inayotaka kuingia kwenye mgogoro na Marekani, hata baada ya kuibuliwa kwa kashfa hii, usiku wa jana ndege iliyomchukua Rais Evo Morales wa Bolivia ilikataliwa kuruka kwenye anga za mataifa kadhaa ya Ulaya, kufuatia uvumi kwamba Snowden alikuwamo kwenye ndege hiyo.
Kuna wengine wanaoamini kwamba hasira zinazoelezewa kuwapo miongoni mwa wanasiasa barani Ulaya zimetiwa chumvi mno, ingawa suala la nini Marekani inafanya na kiwango kikubwa cha taarifa inachokusanya kutoka Ulaya linagusa upande wa kiuchumi pia.
Hans Michelbach, kiongozi wa wabunge wa CSU, amesema kwamba kuna zaidi ya siasa kwenye suala hili, kwani Marekani inafahamu kuwa Umoja wa Ulaya hauungi mkono magaidi, lakini ni mshindani mkubwa kwenye soko la dunia.
Kwa mujibu wa Michelbach, hilo linazusha wasiwasi kwamba sio tu taasisi za serikali za Ujermani na Ulaya zinachunguzwa, bali pia kampuni na taasisi za kibiashara, na hivyo kuipatia Marekani fursa isiyo ya haki kwenye biashara.“
Tayari Waziri wa Maslahi ya Watumiaji wa Ujerumani, Ilse Aigner, ameshaonya kwamba kutumia kisingizio cha vita dhidi ya ugaidi kunaweza kuziba harakati za kuuhujumu uchumi na serikali kwa wakati mmoja.
Wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema kwamba hujuma za mawasiliano zilizigharimu kampuni za Ujerumani euro bilioni 4.2 mwaka jana pekee.
Mwandishi: Jeniffer Fraczek
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Iddi Ssessanga