1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Ukraine laizamisha manowari ya Urusi

Bruce Amani
14 Februari 2024

Jeshi la Ukraine limesema limeizamisha manowari ya Urusi katika Bahari Nyeusi kwa kutumia droni za majini. Mkuu wa jeshi amesema manowari ya Ceaser Kunikov ilizama karibu na Alupka, katika rasi ya Crimea

https://p.dw.com/p/4cNYz
Manowari ya Urusi ya Ceaser Kunikov
Manowari ya Urusi ya Ceaser Kunikov inayoripotiwa kuzamishwa na droni za majini za UkrainePicha: TASS/IMAGO

Jeshi la Ukraine limesema limeizamisha manowari ya Urusi katika Bahari Nyeusi kwa kutumia droni za majini. Mkuu wa jeshi amesema manowari ya Ceaser Kunikov ilizama karibu na Alupka, mji wa Rasi ya Crimea ambayo ilikwapuliwa na Moscow mwaka wa 2014.

Jeshi la Urusi halijathibitisha ripoti hiyo, na badala yake limesema lilizidungua droni za Ukraine katika Bahari Nyeusi usiku wa kuamkia leo.

Avdiivka ni kitovu cha viwanda katika mkoa wa Donetsk
Makabiliano makali yanaendelea katika mji wa AvdiivkaPicha: Ozge Elif Kizil/AA/picture alliance

Wizara ya ulinzi imesema mifumo ya ulinzi wa angani iliharibu droni 9 zilizorushwa na Ukraine katika maeneo ya Urusi ya Belgorodna Voronezh, Pamoja na Bahari Nyeusi.

Katika mji wa Selydove wa mkoa wa mashariki wa Donetsk, mashambulizi ya makombora kadhaa ya Urusi yamewauwa watu watatu usiku wa kuamkia leo na kuwajeruhi wengine kadhaa na kuharibu hospitali na makaazi ya watu. Hayo ni kwa mujibu wa maafisa wa Ukraine.

Wakati huo huo, Mkuu mpya wa majeshi ya Ukraine Oleksandr Syrskyamesema kuwa hali kwenye uwanja wa mapambano ni tete, kufuatia ziara yake ya mashariki mwa Ukraine na Waziri wa ulinzi Rustem Umerov.

Vikosi vya Urusi katika miezi ya karibuni vimekuwa vikipambana kukikamata kitovu cha viwanda cha Avdiivka na vimekuwa vikipata mafanikio katika mapambano hayo.

Syrsky amesema mazingira ya utendakazi ni magumu sana na yanafadhaisha. Kwa sababu Warusi wanaendelea kuongeza juhudi zao na wana faida katika idadi ya askari. Amesema wanafanya juu chini kumzuia adui kusonga ndani kabisa ya mipaka ya Ukraine na kuyadhibiti maeneo yaliyokamatwa.

Ujerumani: Hatutaiacha Ukraine kwenye vita peke yake

Mji wa Avdiivka uko katika jimbo la Donetsk la Ukraine, ambalo limeshuhudhia mapigano makali ya uvamizi wa Urusi wa karibu miaka miwili na Kremlin inadai kuwa mji huo ni sehemu ya Urusi

Na wakati hayo yakiendelea, mjini Brussels mawaziri kutoka mataifa wanachama wa Jumuiya ya Kujihami – NATO wanakutana leo na kesho kujadili uungaji mkono wao kwa Ukraine katika vita vyake na Urusi.

Mkutano wa leo wa NATO, rasmi, ni mkusanyiko ulioratibiwa na Marekani wa washirika wanaoiunga mkono Ukraine na sio NATO yenyewe. Halafu hafla ya kesho ni mkutano kamili wa ngazi ya mawaziri wa NATO.

Soma pia: Marekani: hakuna mwaliko wa NATO kwa Ukraine katika mkutano wa kilele wa Julai

Mazungumzo hayo katika makao makuu ya NATO mjini Brussels yamegubikwa na rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, ambaye aliwaambia waandishi Habari mwishoni mwa wiki katika kampeni yake kuwa anaweza kuihimiza Urusi kufanya chochote kile wanachotaka kwa nchi za NATO ambazo hazina bajeti kubwa ya ulinzi.

afp, dpa, ap, reuters