1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yakataa mazungumzo na Trump

Isaac Gamba
1 Agosti 2018

Maafisa waandamizi wa Iran wamelikataa wazo la rais wa Marekani Donald Trump  la kutaka mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo pasipo masharti yoyote na kusema halina msingi wowote na ni udhalilishaji.

https://p.dw.com/p/32QGE
Iranischer Präsident Hassan Rouhani
Picha: Getty Images/M. Gruber

Waziri wa mambo ya nje wa Iran  ameonya kuwa hatua hiyo  Trump wanayoitafsiri kama ni njia ya kujitengenezea umaarufu haitafanikiwa.

Kwa upande mwingine rais wa Iran Hassan Rouhani alisema uamuzi wa rais Donald Trump kiondoa Iran katika makubaliano ya kimataifa ya nyukilia ulikuwa kinyume cha sheria na kuwa Iran haiko tayari kukubali kirahisi kuruhusu juhudi za Marekani za kutaka kuvuruga uchumi wa nchi hiyo unaotokana na mafuta.

Hayo yanajiri huku rais Donald Trump akisisitiza kuwa mazungumzo kati  yake na   viongozi wa Iran lazima  yafanyike  huku akiongeza kuwa ana hisia  Iran itakuwa na mazungumzo na Marekani hivi karibuni.

Trump amerudia kauli  yake kuwa makubaliano ya nyukilia kati ya Iran na mataifa yenye nguvu yaliinufaisha zaidi Iran na kuwa kwa sasa Iran iko katika wakati mgumu mnamo wakati Marekani ikitarajia kuiwekea vikwazo zaidi Iran  kuanzia Agosti 6 mwaka huu.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema kuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo naye  anaunga mkono hoja ya Trump ya kutaka kuwa na mazungumzo na maafisa wa Iran.

Mnamo mwezi Mei mwaka huu Trump aliiondoa Marekani katika makubaliano hayo ya kimataifa ya nyukilia akidai mkataba huo unainufaisha zaidi Iran mnamo wakati Jumatatu wiki hii akitangaza kuwa yuko tayari kukutana na rais Hassan Rouhani wa Iran pasipo masharti ili kujadili jinsi ya kuimarisha mahusiano.

 

Iran yasema Marekani ijilaumu yenyewe

USA - Präsident Donald Trump beim Treffen mit Guiseppe Conte
Rais Donald Trump wa MarekaniPicha: picture alliance/AP Photo/E. Vucci

Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif  kupitia ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter alisema Marekani itapaswa kujilaumu yenyewe kwa kusitisha mazungumzo na Iran wakati ilipojitoa kwenye makubaliano ya nyukilia huku akisisitiza kuwa vitisho, vikwazo na hatua zake za kutaka kujitengenezea umaarufu hazitafanikiwa.

Msemaji wa wizara ya mambo yanje ya Iran amesema wazo la  rais Donald Trump la kutaka mazungumzo na Iran  pasipo masharti haliendani na vitendo vya kiongozi huyo kutokana na vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran pamoja  na kuziwekea mbinyo nchi nyingine ili zifanye biashara na Iran.

Ama kwa upande wake kiongozi wa jeshi katika Jamhuri ya kiisilamu ya Iran Mohammad Ali Jafari alikaririwa akimueleza rais Trump kuwa Iran sio Korea Kaskazini ambayo inaweza kukubali wazo lake la kukutana naye kwa ajili ya mazungumzo.

Naye mkuu wa baraza la kimkakati la Iran kuhusiana na masuala ya uhusiano wa kimataifa  Kamal Kharrazi  alisema Iran haioni maana yoyote juu ya kufanya mazungumzo na Trump mnamo wakati ni wiki moja tu tangu Trump alipoionya Iran kuwa inakabiliwa na hatua kali iwapo itatoa vitisho dhidi ya Marekani na hasa ukichukulia pia rekodi ya maafisa wa Marekani mara kadhaa ya kukiuka makubaliano.

Makundi yenye msimamo mkali nchini Iran na ambayo yalipinga makubaliano hayo ya nyukilia kwasasa yanaonekana kuungana na serikali kupinga hatua hiyo ya sasa ya rais Trump.

Mwandisi: Isaac Gamba /RTRE/AFPE

Mhariri: Josephat Charo