Intaneti kama injini ya maendeleo Afrika | Makala | DW | 16.11.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Makala

Intaneti kama injini ya maendeleo Afrika

Umuhimu wa intaneti katika maedeleo barani Afrika, nafasi ya wanawake katika siasa za bara hilo na hofu ya mataifa ya Afrika kuhusu vita vya kibishara vya rais Donald Trump ndani ya Afrika katika magazeti ya Ujerumani.

Gazeti la Frankfurter Allgemeiner lililoripoti juu ya umuhimu wa intaneti katika kusukuma mbele maendeleo barani Afrika. Gazeti hilo linaangazia mkakati wa waziri wa ushirikiano wa kimaendeleo wa Ujerumani Gerd Müller ambaye wizara yake inayatafutia fursa za uwekezaji katika teknolojia ya kidigitali barani Afrika, makampuni yapatayo 130.  Kupitia mradi wa ushirikiano wa kimkakati wa kidijitali na Afrika, inaelezwa kuwa tayari euro milioni 150 zimetengwa kwa ajili ya miradi 40.

Kwa mujibu wa wizara hiyo hata hivyo, fedha hizo ni kidogo sana. Wizara ya ushirikiano wa kimaendeleo inazingatia hasa ushirikiano na kampuni za Kijerumani na vikundi vya wabunifu Afrika. Kimsingi, mageuzi ya kidijitali yanafungua fursa mpya katika nyanja za biashara. Nchini Rwanda kwa mfano, Wajerumani wanafanyia kazi mradi wa ushirikishanaji magari. Kampuni za Volkswagen, Siemens na SAP ziko njiani.

Uimarishwaji wa mifumo ya afya ya kidijitali unatazamwa na Berlin kama jukumu muhimu, linaandika gazeti la Frankfurter Allgemeiner, na kuzungumzia vifo vipatavyo milioni 1.6 ambavyo linasema vingeweza kuzuwilika kupitia mfumo wa afya unaofanya kazi vizuri.

Matumaini yanawekwa kwenye mifumo ya maonyo ya mapema pia kuweza kuzuwia majanga na miripuko kabla havijatokea. Zaidi ya hayo, ndege za kuendesha kwa rimoti zitatumiwa kusafirisha dawa na damu vinavyohitajika haraka katika maeneo yasiyofikika kwa urahisi. Katika hili kuna mradi unaoendeshwa na DHL nchini Tanzania.

Meaza Ashenafi (Federal Government Communication Affairs Office of Ethiopia )

Ethiopia imeingia katika orodha ya mataifa yenye idadi kubwa ya wananwake wengi katika nafasi za uongozi.

Kupitia shirika la utengenezaji ndege la Airbus, Ujerumani inataka kuvisaidia vikundi vya ubunifu vinavyofanyakazi kufikisha mawasiliano ya intanet katika maeneo ya vijijini barani Afrika. Kwa mujibu wa ufafanuzi uliotolewa na serikali mjini Berlin, upatikanaji wa intaneti kwa ngazi ya mataifa yalioendelea kiviwanda, unaweza kuunda nafasi za ajira zipatazo milioni 140 katika mataifa yanayoendelea. Hilo lakini litahitaji ugavi bora wa nishati. Hivi sasa asilimia 60 ya wakaazi wa bara la frika wanaishi bila umeme.

Siasa za Afrika zinazidi kuwakumbatia wanawake

Gazeti la Neue Zürcher Zeitung limeandika juu ya siasa za Afrika, likiangazi viunzi vinavyoendelea kuwakabili wanawake katika juhudi zao za kuzifikia nafasi za juu za uogozi barani humo. Likiwa na kichwa cha habari kisemacho: Siasa za Afrika zinazidi kuwakumbatia wanawake, gazeti hilo linuangazia mkutano wa kilele kati ya China na Afrika uliofanyika mwezi Septemba ambako hakukuwa na mwanamke hata mmoja miongoni mwa viongozi wakuu wa nchi waliokusanyika mjini Beijing.

Hali hiyo, linasema gazeti la Neue Zürcher Zeitung, inamfanya mtu kuamini kuwa siasa katika kanda ya kusini mwa jangwa la Sahara ni kazi ya wanaume tu. Kwa muda mrefu kulikuwa na ishara ndogo sana kwamba hilo lingeweza kubadilika.

Katika siku za karibuni hata hivyo kumekuwa na ishara katika mataifa kadhaa kwamba udhibiti wa wanaume katika siasa za bara hilo unaanza kuporomoka. Katikati mwa mwezi Oktoba, waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed aliteuwa baraza jipya la mawaziri, nusu yake wakiwa ni wanawake. Siku kadhaa baadaye, bunge la taifa hilo lilimchaguwa rais wa kwanza mwanamke katika eneo la pembe ya Afrika.

Karibu wakati sawa na huo, rais wa Rwanda Paul Kagame alitangaza kuwa wanawake watashika asilimia 50 ya nyadhifa za uwaziri katika serikali yake. Gazeti hilo linawataja pia wanawake kadhaa waliochaguliwa katika nayadhifa mbalimbali za juu katika mataifa ya Afrika, na kunukuu takwimu zinazoonyesha namna wanasiasa wanawake wanavyozidi kuwa maarufu na kukubalika barani Afrika.

USA | Donald Trump spricht vor Medien (picture-alliance/dpa/CNP /MediaPunch/R. Sachs )

Rais wa Marekani Donald Trump.

Afrika yahofia vita vya biashara vya Trump

Gazeti la Handelsblatt limeripoti juu ya hofu ya mataifa ya afrika, namna vita vya kibishara ya Marekani na China vinavyoweza kuathiri ukuaji wake. Linasema waathirika wakubwa wa mgogoro wa kibiashara kati ya Marekani na China ni mataifa madogo na maskini zaidi, ambayo hakuna anaeyafikiria.

Handelsblatt linamkunukuu Dirk Kohnert kutoka taasisi ya masuala ya Afrika ya mjini Hamburg, ambaye anasema Afrika inategemea zaidi biashara ya nje kuliko Ulaya, ambako asilimia 63 ya biashara hufanyika ndani ya kanda hiyo. Kohnert aliandika hayo katika makala yake iliochapishwa katika jarida la Tathmini ya uchumi wa kisiasa barani Afrika.

Kutokana na udhaifu wake kiuchumi, mataifa ya Afrika yako mbali kwenye orodha ya washirika muhimu wa kibiashara wa Marekani.Lakini kwa Misri na Afrika Kusini, mauzo ya bidhaa za chuma nchini Marekani yanachangia pakubwa kwenye uchumi wao. 

Mataifa madogo yanayoendelea yanakuwa mlengwa wa moja kwa moja wa vikwazo pale maslahi ya Marekani yanapotishiwa, anásema Kohnert na kutolea mfano wa mataifa ya Kenya, Uganda, Tanzania na Rwanda, ambayo yalikuwa yameamua kupiga marufuku uingizaji wa nguo za mitumba kuanzia mwaka 2019 ili kulinda viwanda vyake vya ndani. Matokeo yake ni kwamba Marekani ilitishia kuondoa upendeleo wa kodi kwa mataifa hayo. Matatu kati yake yakasalimu amri.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman