1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Idadi ya vifo, majeruhi wa miripuko ya Beirut yapanda

5 Agosti 2020

Waokoaji nchini Lebanon wameendelea kufukuwa vifusi kujaribu kuwatafuta manusura wa miripuko miwili mikubwa kwenye ghala la kemikali iliyoutikisa mji mkuu Beirut, ikiwauwa watu 78 na kuwajeruhi wengine wapatao 4,000.

https://p.dw.com/p/3gQUO
Libanon | Gewaltige Explosion in Beirut
Picha: AFP via Getty Images

Maafisa wa serikali walisema kuwa huenda idadi ya vifo na majeruhi ingeliongezeka wakati jitihada za uokozi zikiendelea.

Miripuko hiyo miwili kwa pamoja jioni ya Jumanne (Agosti 4) ilitokea kwenye ghala linalohifadhi vitu vinavyoripuka katika bandari ya Beirut inatajwa kuwa mikubwa kabisa kuwahi kutokea kwa miaka kadhaa.

Rais Michel Aoun alisema kwamba tani 2,750 za kemikali ya ammonium nitrate, inayotumika kwa ajili ya mbolea na mabomu, zilikuwa zimehifadhiwa kwa miaka sita kwenye bandari hiyo bila ya kuwekewa taratibu za kiusalama, jambo aliloliita kwamba "halikubaliki." 

Rais huyo aliitisha mkutano wa dharura wa baraza la mawaziri siku ya Jumatano (Agosti 5). Waziri Mkuu Hassan Diab aliahidi kwamba kutakuwa na uwajibikaji kutokana na miripuko hiyo na kwamba waliohusika "watachukuliwa hatua kali."

Maafisa wa serikali hawakusema kipi hasa kilisababisha moto uliochochea miripuko hiyo, lakini chanzo kimoja cha usalama na vyombo vya habari vya Beirut vilisema cheche za moto zilitokana na wafanyakazi wa kuchomelea vyuma waliokuwa wakiziba tundu kwenye ghala hilo.

"Tunashuhudia janga kubwa sana," mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Lebanon, George Kettani, alikiambia kituo cha utangazaji cha Mayadeen. "Kuna maiti na majeruhi kila mahala."

Hata baada ya kupita masaa kadhaa tangu mripuko huo, ambao ulitokea saa 12:00 jioni, moto ulikuwa bado unawaka kwenye eneo hilo, ukiunda wingu la manjano kwenye anga, huku sauti za helikopta na magari ya uokozi zikisikika kwenye mji huo mkuu. 

Trump asema yalikuwa mashambulizi

Libanon | Gewaltige Explosion in Beirut
Sehemu ya hasara kutokana na mripuko mkubwa wa Beirut.Picha: AFP via Getty Images

Licha ya ripoti za awali kutoka kwa viongozi wa Lebanon kuhusisha miripuko hiyo na ghala la kemikali, Rais Donald Trump wa Marekani aliwaambia waandishi wa habari kwamba majenerali wa kijeshi wa nchi yake walimuambia kuwa "walikuwa wanahisi mripuko huo yalikuwa mashambulizi ya bomu."

"Nilikutana na baadhi ya majenerali wetu wakubwa na wanaonekana kuhisi lilikuwa bomu. Mripuko huu haukuwa tukio la aina fulani ya miripuko ya kemikali za kutengeneza. Wanaonekana kudhani kwamba yalikuwa mashambulizi. Kitu kama bomu hivi," alisema kiongozi huyo wa taifa lenye ukaribu mno na Israel, jirani hasimu wa Lebanon. 

Wakaazi wengine walifikiri kuwa tetemeko la ardhi lilikuwa limeipiga nchi hiyo. Kwa mujibu wa Kituo cha Sayansi ya Miamba cha Ujerumani, miripuko hiyo ilisababisha tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 3.5 kwa vipimo vya Richter na ulisikika hadi nchini Cyprus, umbali wa kilomita 200 kuvuuka Bahari ya Mediterenia.  

Israel yajitenga kando, yaahidi msaada

Libanon | Gewaltige Explosion in Beirut
Madhara ya miripuko ya Beirut.Picha: Getty Images/AFP/M. Tahtah

Miripuko hiyo iliyotokea wakati mzozo kati ya Israel na kundi la Hizbullah nchini Lebanon ukiendelea kwenye mpaka wa kusini, ilirejesha kumbukumbu za vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1975 hadi 1990, ambapo Lebanon ilishuhudia miripuko mikubwa mikubwa, mabomu ya kutegwa garini na mashambulizi ya anga ya jeshi la Israel. 

Baadhi ya wakaazi wengi walisema walisikia mivumo ya ndege muda mfupi kabla ya miripuko hiyo, lakini maafisa wa Israel walijitenga kando na miripuko hiyo, na badala yake walisema nchi yao iko tayari kutoa msaada wa kibinaadamu na matibabu. 

Iran, muungaji mkono mkubwa wa Hizbullah, pia iliahidi kutoa msaada, ahadi ambayo pia ilitolewa na hasimu wake mkubwa kwenye eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati, Saudi Arabia. 

Miripuko hiyo ilitokea siku tatu tu kabla ya mahakama inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kutowa hukumu yake kwenye kesi ya washukiwa wanne kutoka kundi la Hizbullah, ambao wanatuhumiwa kufanya mashambulizi ya bomu ya mwaka 2005 yaliyomuua Waziri Mkuu Rafik al-Hariri na watu wengine 21. 

Hariri aliuawa kutokana na mripuko mkubwa wa bomu kwenye eneo ukingo huo huo wa maji, umbali wa kilomita mbili kutoka bandarini.