Hatimaye Maalim Seif aruhusiwa kuwania urais wa Zanzibar | Matukio ya Afrika | DW | 11.09.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

UCHAGUZI MKUU ZANZIBAR 2020

Hatimaye Maalim Seif aruhusiwa kuwania urais wa Zanzibar

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ilimtangaza kiongozi huyo mashuhuri wa upinzani kwamba amepitishwa kuwania kiti cha urais mara baada ya kumaliza kusikiliza pande zilizohusika na pingamizi aliyokuwa amewekewa.

Baada ya zaidi ya takribani masaa 24 ya wasiwasi na taharuki miongoni mwa wafuasi wa upinzani visiwani Zanzibar, hatimaye Tume ya Uchaguzi ya visiwa hivyo vya Bahari ya Hindi  ilimtangaza Maalim Seif Sharif Hamad kuwa mgombea halali kwenye uchaguzi wa tarehe 27 na 28 Oktoba mwaka huu kupitia chama cha ACT Wazalendo.

Barua iliyosambazwa mitandaoni na maafisa wa chama hicho inaeleza kuwa Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Mkuu Mstaafu Hamid Mahmoud, alikuwa amemteuwa rasmi Maalim Seif na hapo hapo kumruhusu kuendesha kampeni zake. 

Mwanasheria mkuu wa ACT Wazalendo, Omar Said Shaaban, aliwaambia waandishi wa habari kwamba uamuzi wa ZEC ulizingatia kuwa kile kilichoitwa "taarifa za uongo" kwenye fomu za uteuzi za mteja wake hazikuwa na mashiko kwa kuwa hata kama zingelikuwa za kweli, basi hazikulenga kumnufaisha mgombea huyo.

Uamuzi huo uliotangazwa jioni ya takribani saa 12:00 kwa majira ya Afrika Mashariki, ulimfanya Maalim kuwa mtu wa 17 na wa mwisho kutangazwa kuwania kiti hicho kwenye uchaguzi wa Oktoba 2020.