Gauck ataka Wajerumani waendeleze ukarimu kwa wageni | Masuala ya Jamii | DW | 24.12.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Gauck ataka Wajerumani waendeleze ukarimu kwa wageni

Rais Joachim Gauck wa Ujerumani anasema mijadala ya wazi ndiyo yatakayoleta suluhisho linaloakisi maadili sio kuhatarisha mafungamano ya kijamii kati ya wenyeji na wahamiaji barani Ulaya.

Rais Joachim Gauck wa Shirikisho la Ujerumani.

Rais Joachim Gauck wa Shirikisho la Ujerumani.

Akizungumza kupitia hotuba yake ya Krismasi kwa kwa taifa usiku wa kuamkia leo (tarehe 24 Disemba), Rais Gauck aliwakumbusha Wajerumani kwamba maandiko matakatifu ya Kikristo yanaonesha matukio yanayoadhimishwa kwenye Krismasi ni ishara ya mapenzi ya Mungu kwa ulimwengu na karama yake.

"Ni jambo jema mno kuneemewa kwa karama hii, lakini ni vyema zaidi kama tunaweza kuiingiza karama hii kwenye maisha yetu na kuisambaza kwa walimwengu wengine," alisema Rais Gauck, ambaye aliwahi kuwa mchungaji wa kanisa na mwanaharakati wa haki za binaadamu.

Rais Gauck alitumia pia hotuba hiyo kuwashukuru wale wote walioisaidia Ujerumani kukabiliana na wimbi la wakimbizi, wakiwamo wafanyakazi wa kujitolea. "Tumeonesha kwamba tunao uwezo, kwa maana ya dhamira njema na utaalamu na pia kwenye sanaa ya uimarishaji uwezo wetu," alisema, akiongeza kwamba kujitokeza kwa watu wengi waliojitolea wenyewe kusaidia kumeigeuza Ujerumani kuwa nchi ya "wenye moyo wa huruma na ukarimu."

Ubishani kama 'sehemu ya demokrasia'

Gauck alizungumzia pia kuwepo kwa mdahalo wa kina unaoendelea nchini Ujerumani hivi sasa juu ya namna ya kuwashughulikia wale wanaoomba hifadhi. "Vipi tunapaswa kuwashughulikia wakimbizi wanaotafuta mahala pa kukaa na mustakabali wa maisha yao nchini mwetu?"

Pendekezo la Rais Gauck ni kwamba ni kupitia mijadala na midahalo ya wazi tu "ndipo tunaweza kupata suluhisho lenye maana ambalo litaungwa mkono na walio wengi." Mabishano yaliyopo kwenye suala lenyewe si kuharibika kwa umoja wa Ujerumani, alisema, bali ni sehemu ya maisha kwenye demokrasia. Aliwasifu wananchi kwa namna wanavyojihusisha na masuala ya kisiasa katika kusaidia kuyazusha masuala ambayo hayajapatiwa ufumbuzi.

Hata hivyo, Rais Gauck, ambaye mwenyewe alikulia mashariki mwa Ujerumani ambako sasa kumekuwa kitovu cha chuki dhidi ya wageni, alisema mashambulizi na chuki hizo si njia halali za kutatua matatizo na kutoa wito wa kuangaliwa mambo hayo kwa umakini mkubwa.

"Lazima sasa ipatikane suluhisho inayoakisi vigezo vya kimaadili na sio vinavyohatarisha utangamano wa kijamii na ambavyo vinazingatia ustawi wa raia wetu wenyewe bila kusahau masaibu ya wakimbizi", alisema Gauck akiongeza kwamba raia na wanasiasa lazima wailinde misingi ya kiliberali na kidemokrasia inayoifanya Ujerumani kuwa "nchi inayopendwa na iliyo mahala pema pa kuishi."

Khofu na ukosefu wa usalama

Akizungumzia mwaka unaomalizika wa 2015, Rais Gauck alisema ulikuwa mwaka uliojaa mashaka na wasiwasi wa ghasia, ugaidi na vita, mambo ambayo yamepandikiza khofu na hali ya kutojihisi salama. Migogoro kadhaa ilitokea kwenye mwaka huu, huku mingine bado ikiendelea hadi sasa: mzozo wa kifedha, kuongezeka tafauti ndani ya Umoja wa Ulaya na mdahalo juu ya mustakabali wa Ugiriki.

Gauck alizungumzia pia mizozo nchini Ukraine, Syria, Afghanistan na sehemu kadhaa barani Afrika zilizoathiriwa na ugaidi.

Katika hotuba hiyo iliyorikodiwa kwenye makaazi yake rasmi ya Schloss Bellevue jijini Berlin, Rais Gauck aliwatakia pia kheri wanajeshi wa Ujerumani waliotumwa kwenye maeneo "hatari kupambana dhidi ya mizizi ya ugaidi."

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa
Mhariri: Bruce Amani

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com