1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan kukutana tena na Putin kuhusu Ukraine

Sudi Mnette
Liochapishwa 5 Agosti 2022ilisahihishwa mwisho 5 Agosti 2022

Wakati viongozi wa Urusi na Uturuki wanatarajiwa kukutana leo hii kwa ajili ya mazungumzo ya kumaliza vita vya Ukraine. Mapigano yanaendelea Donetsk huko Mashariki mwa Ukraine.

https://p.dw.com/p/4FAcC
Iran Russland Türkei | Dreiergipfel | Wladimir Putin, Ebrahim Raisi und Recep Tayyip Erdogan
Picha: Sergei Savostyanov/TASS/dpa/picture alliance

Kimsingi mazungumo ya leo ya mjini Sochi ya Rais Vladimir Putin na mwenzake wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, vita hivyo vya Ukraine na hali ilivyo Syria ni miongoni mwa masuala yatakayopewa nafasi kubwa. Katika muktadha huo kiongozi huyo wa Uturuki atafanya jitihada ya kiwango cha juu ya kidiplomasia kwa lengo la kufanikisha usafirishaji wa nafaka ya Ukraine kupitia Bahari Nyeusi.

Ni awamu ya pili ya mazungumzo baina ya viongozi hao katika kipindi cha siku 17 tu. Lakini wana mvutano wao, itakumbukwa mwezi uliopita mjini Tehran Putin alimwambia Erdogan kwamba taifa lake linapinga shambulizi lolote linalopangwa dhidi ya wapiganaji wa Kikurd kule Kaskazini mwa Syria.

Tofauti za Erdogan na Putin

Wachambuzi wanasema tofauti hizo zimekuwa zikichagiza mahusiano kati ya mataifa hayo mawili kwa takribani miaka 20 ssasa,ingawa hii vita ya sasa ya Ukraine na Urusi imeipa Uturuki muonekano mwingine na kumpa Erdogan umuhimu mkubwa kuliko wakati mwingine wowote katika kipindi cha miaka michache iliyopita.

Andiko la juma lililopita la afisa mwandamizi anaehusika na masuala ya kigeni wa Baraza la Ulaya, Asli Aydintansbas linasema idadi kubwa ya raia wa Uturuki wanaunga mkono msimamoo wa kutoegemea upande wowote kati ya Urusi na Mataifa ya Magharibi.

Meli tatu za nafaka zaondoka Ukraine

Ukraine "Navistar" verlässt den Haffen von Odessa
Meli ya nafaka ikitoka bandari ya OdessaPicha: Turkish National Defense Ministry Press Office/TASS/picture alliance/dpa

Wakati jitihada hiyo ya upatanishi ikisubiriwa meli tatu za nafaka zimeondoka mapema leo katika banadari za Bahari Nyeusi za Odessa na Chornomorsk. Habari hii imethibitishwa na Waziri wa Miundombinu wa Ukraine,  Olexandr Kubra kupitia ukurasa wake wa telegramu. Amesema meli ya mwanzo kutoka Grater Odessa ina tani 57,000 za mahindi.

Safari hizi ni kwa mujibu wa makubaliano ya safari salama ya Julai 22. Na kwa mujibu wa serikali ya Ukraine meli hizo kwanza zitatia nanga Istanbul kwa ukaguzi na baadae kuelekea Uingereza na Ireland. Katika hatua nyingine Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amekosa ripoti ya shirika la utetezi wa haki za binaadamu la Amnesty International kwa kuainisha ukikukwaji wa haki za binaadamu ndani ya taifa lake."Tumeshuhudia leo ripoti tofauti kabisa ya Amnesty International, ambayo kwa bahati mbaya inajaribu kutoa msamaha kwa serikali ya kigaidi na kuhamisha jukumu kutoka kwa mchokozi hadi kwa mwathirika."

Soma zaidi:UN yataka kukagua kinu cha nyuklia cha Ukraine

Katika uwanja wa mapambano Urusi majeshi ya Urusi yameanzisha mashambulizi makali katika eneo la Donetsk, ambapo habari za sasa zinasema kwa ushirikiano na wapiganaji wanaotaka kujitenga wamefanikiwa kukidhibiti kijiji kimoja cha eneo hilo kiitwacho Pisky. Shirika la habari la TASS limesema kadhalika mapigano yanaendelea katika mji wa Bakhmut, huko kaskanini mwa Donetsk.

Serikali ya Urusi ipo katika jitihada za kutaka kuyadhibiti maeneo ambayo wakazi wake wengi wanazungumza Kirusi, kama Donbas, yenye kujumuisha majimbo ya Luhansk na Donetsk, ambapo wanaotaka kujitenga na kuegemea upande wa Urusi yameyateka maeneo hayo.

Vyanzo: DPA/RTR