Dunia yatoa wito wa amani kati ya Marekani na Iran
12 Aprili 2026
Viongozi mbalimbali duniani wamezitaka Marekani na Iran kuendelea na mazungumzo baada ya mazungumzo marefu kati ya Washington na Tehran mjini Islamabad kumalizika Jumapili bila makubaliano ya kumaliza vita Mashariki ya Kati.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, ameitaka Marekani na Iran kutafuta suluhu akisisitiza umuhimu wa kuendeleza usitishaji mapigano na kuepuka kuongeza mvutano.
Katika taarifa ya mazungumzo ya simu kati ya Starmer na Sultani Haitham bin Tarik al Said wa Oman, msemaji wa Starmer amesema viongozi hao pia wamejadili kufunguliwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, ambao kufungwa kwake kumepandisha bei za nishati.
Waziri wa mambo ya nje wa Pakistan, Ishaq Dar, amesema wataendelea kusaidia juhudi za mawasiliano kati ya Iran na Marekani.
Umoja wa Ulaya umesisitiza umuhimu wa diplomasia huku rais wa Urusi Vladimir Putin akisema yuko tayari kusaidia juhudi za kutafuta suluhu ya kisiasa na kidiplomasia kufikia amani ya kudumu Mashariki ya Kati.
Kauli hizi zinatolewa wakati Uingereza ikijiandaa kuongoza mikutano zaidi ya kimataifa wiki ijayo ili kushinikiza amani, kuhakikisha usafirishaji baharini unaendelea, na kupunguza mzozo kati ya mataifa husika.