1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha CUF Tanzania chataka uchaguzi usivurugwe na dola

6 Oktoba 2025

Mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Tanzania cha Wananchi CUF Profesa Ibrahim Lipumba ametoa wito wa mchakato wa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba kutoingiliwa na vyombo vya dola.

https://p.dw.com/p/51Xsa
Tanzania Dar es Salaam | Chama cha CUF | Ibrahim Lipumba
Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha wananchi CUF nchini Tanzania, Profesa Ibrahim Lipumba ametaka mchakato wa uchaguzi mkuu wa 2025 kutoingiliwa na dolaPicha: DW/S. Khamis

Chama hicho kimemuomba Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni mgombea wa chama tawala CCM kuwahakikishia wananchi kuwa maoni yao yataheshimiwa kupitia sanduku la kura kwa tume ya uchaguzi kutenda haki. 

Lipumba aliyewahi kuwania urais zaidi ya mara tatu amesema licha ya mazingira kutokuwa rafiki kwa vyama vya upinzani lakini chama chake kimeamua kushiriki uchaguzi kama hatua ya kizalendo, akisisitiza ukuzaji wa demokrasia ni mchakato unaopitia safari ndefu.

Amesema Rais Samia anapaswa kuweka mazingira ya ukweli na uwazi katika uchaguzi na kusisitiza mgombea atayechaguliwa ndiye anayepaswa kutangazwa bila ya vyombo vingine kuingilia mchakato huo.

Tanzania Arusha | Mgombea wa urais nchini Tanzania kupitia chama tawala CCM- Samia Suluhu Hassan
Mgombea wa urais nchini Tanzania Samia Suluhu Hassan akizungumza kwenye moja ya mikutano ya kampeni nchini humoPicha: CCM

"Afisa wa jeshi" azua tafrani

Hivi karibuni mtu aliyejitambulisha kuwa afisa wa jeshi la wananchi JWTZ na kujitambulisha kama Kapteni Tesha kuzungumza kupitia mitandao ya kijamii na kuzua mjadala imezidi kuibua makundi ya watu na safari hii mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Joseph Butiku ameonya juu ya kutoliingiza jeshi hilo katika masuala ya siasa ili kuepusha balaa.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Mjini Musoma, mkongwe huyo wa siasa amesema haamini kama "Tesha" ni mwanajeshi na kauli yake imelenga tu kuvuruga mshikamano wa kitaifa.

Jeshi la Polisi nchini humo limeonya vikali dhidi ya wale wanaotengeneza na kusambaza taarifa za uchochezi. Msemaji wake David Misime amesema jeshi hilo linafuatilia nyendo za wahusika na litawafikisha kwenye mkono wa sheria.

Tanzania inajiandaa na Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 huku chama kikuu cha upinzani kujiweka kando na uchaguzi huo kikishinikiza kufanyika marekebisho yanayomulika mazingira ya uchaguzi.