Bunge la Uingereza laridhia muswada tata wa Boris Johnson | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.09.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Muswada tata wa Johnson wavuka kiunzi cha bunge

Bunge la Uingereza laridhia muswada tata wa Boris Johnson

Muswada wa waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson unaokiuka vipengele vya makubaliano na Umoja wa Ulaya juu ya Uingereza kuondoka katika umoja huo, umevuka kiunzi kingine baada ya kuungwa mkono na bunge.

England | House of Commons | Brexit Debatte | Boris Johnson

Bunge la Uingereza limeridhia muswada tete wa Waziri Mkuu Boris Johnson

Wabunge wa Uingereza waliuridhia muswada huo juu ya soko la ndani la Uingereza, baada ya waziri mkuu Boris Johnson kuufanyia marekebisho, na kukubali matakwa ya wabunge waasi ndani ya chama chake cha Conservative, kwamba bunge litakuwa na kauli ya mwisho ya kuidhinisha vipengele vinavyokwenda kinyume na makubaliano yaliyosainiwa baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya.

Soma zaidi: Umoja wa Ulaya waionya Uingereza kuhusu mktaba wa Brexit

Baada ya ridhaa hiyo ya bunge ambayo haikupigiwa kura rasmi, serikali ya Johnson imesema kinachofuata ni utaratibu utakaoanza leo wa wabunge kuuchunguza kwa kina muswada huo wenye utata.

Kinga ya kisheria kukiuka vipendele asivyovikubali

England | House of Commons | Brexit Debatte | Boris Johnson

Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza

Waziri mkuu huyo wa Uingereza anaendeleza mchakato wa kuufanya muswada huo kuwa sheria, akikaidi maonyo kutoka Umoja wa Ulaya, Jamhuri ya Ireland, Ireland ya Kaskazini na hata kutoka ndani ya chama chake mwenyewe, kwamba sheria hiyo itahujumu mazungumzo magumu yanayoendelea kuhusu uhusiano wa baadaye kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya.

Johnson ananuia kuweka kile anachokiita ''Kinga ya usalama kisheria'', atakayoitumia kukiuka kipengele chochote kinachoweka kanuni tofauti za kiushuru kati ya Ireland ya Kaskazini na sehemu zilizobaki za Uingereza.

Soma zaidi: Mpango wa Uingereza wa Brexit waibua wasiwasi Umoja wa Ulaya

Vipengele hivyo viliwekwa katika makubaliano yaliyosainiwa awali, kwa lengo la kuepusha ukaguzi kwenye mpaka kati ya Jamhuri ya Ireland na Ireland ya Kaskazini, sehemu ya kisiwa cha Ireland ambayo pamoja na Uingereza itaondoka katika Umoja wa Ulaya.

Mawaziri wa Ulaya waghadhabishwa

Karte Irland Nordirland Kinawley Cornafean EN

Mpaka kati ya Jamhuri ya Ireland na Ireland ya Kaskazini ndio mzizi wa fitina

Waziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Ireland Simon Coveney ambaye amekutana na maafisa waandamizi wa Umoja wa Ulaya, amesema mienendo ya Uingereza inaleta wasiwasi mkubwa miongoni mwa washirika wa Umoja wa Ulaya.

''Kinachotia wasiwasi mnamo siku mbili zilizopita, kwa mujibu wa ninayoyasikiwa kutoka kwa mawaziri wenzangu wa Ulaya, ni hisia zinazoongezeka kuwa Uingereza haitaki makubaliano, na muswada huu ni kisingizio cha kulaumiana baada ya mazungumzo kushindwa.'' Amesema Coveney na kuongeza kuwa yeye amewahakikishia mawaziri wenzake kuwa Uingereza inataka makubaliano, ingawa inatumia njia za kushangaza kutaka kuyafikia.

Hapo jana, naibu waziri wa Ujerumani anayeshughulikia masuala ya Ulaya Michael Roth aliitolea wito Uingereza kuheshimu makubaliano iliyoyatia saini, na kuongeza kuwa muswada huo wa soko la ndani wa serikali ya Johnson unaupa Umoja wa Ulaya wasiwasi mkubwa, kwa sababu unavunja kanuni muhimu za makubaliano ya Uingereza kuondoka katika Umoja wa Ulaya, na hilo, alionya waziri Roth, halikubaliki hata chembe.

 

dpae, afpe