1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden, Trump na kampeni za uchaguzi wa katikati ya muhula

Grace Kabogo
7 Novemba 2022

Rais wa Marekani, Joe Biden na rais wa zamani Donald Trump wamefanya kampeni zao za mwisho mwisho siku mbili kabla ya kufanyika uchaguzi wa bunge wa katikati ya muhula nchini Marekani.

https://p.dw.com/p/4J8uI
USA Wahlkampf Midterm Barack Obama Joe Biden
Picha: Patrick Semansky/AP Photo/picture alliance

Uchagzu huo utaelezea muda uliosalia wa rais wa Marekani na unaweza kufungua njia kwa Trump kurejea katika Ikulu ya White House.

Chama cha Democratic cha Rais Biden kinapambana kundelea kulidhibiti Bunge la Marekani, baada ya uchaguzi ambao Biden amesema utaamua hatma ya demokrasia ya Marekani, ingawa masuala kama vile mfumuko wa bei yalitawala zaidi kampeni hizo.

Biden ameonya kuwa ushindi wa Republican katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika siku ya Jumanne, unaweza kudhoofisha demokrasia ya Marekani.

Biden: 76% wana wasiwasi kuhusu demokrasia

''Sote tunajua kwamba demokrasia yetu iko hatarini. Utafiti wa maoni wa hivi karibuni umeonesha kuwa asilimia 76 ya watu wa Marekani wana wasiwasi kuhusu kudumisha demokrasia yetu. Na tunajua kwamba huu ni wakati wa kizazi chenu kuitetea, kuilinda na kuichagua,'' alisema Biden.

Akifanya kampeni siku ya Jumapili katika jimbo la Florida, Trump kutoka chama cha Republican amewasihi wafuasi wake kumchagua mgombea wa jimbo la Florida, Marco Rubio.

''Siku mbili tu kuanzia sasa watu wa Florida wanamtachagua tena rafiki yangu mkubwa, Marco Rubio kuwa mwakilishi wa Baraza la Senate. Na pia mtamchagua tena Ron DeSantis kuwa gavana wa jimbo lenu,'' alisema Trump.

USA Latrobe Donald J. Trump Auftritt
Rais wa zamani wa Marekani, Donald TrumpPicha: Kyle Mazza/AA/picture alliance

Wagombea wa chama cha Democratic wamekuwa wakipigiwa kampeni na vinara wa chama hicho wakiwemo marais wa zamani wa Marekani, Barack Obama na Bill Clinton.

Utafiti wa maoni ya wapiga kura umeonesha kuwa Wamarekani wengi wana wasiwasi kuhusu uchumi na wanahisi kwamba nchi hiyo iko katika mwelekeo mbaya. Utafiti huo pia unawaweka Warepublican mbele katika kupigania kudhibiti viti katika Baraza la Wawakilishi na pia unaonesha kuwa na nguvu katika Baraza la Seneti.

Huku viti vyote 435 katika Baraza la Wawakilishi vikigombaniwa pamoja na theluthi moja ya wajumbe 100 wa Baraza la Seneti na nafasi kadhaa za majimbo, wanachama wa Democratic wamekuwa wakionesha ujasiri katika matarajio yao.

Warepublican wako katika nafasi nzuri

Warepublican wako katika nafasi nzuri ya kunyakua viti vingi vya bunge katika uchaguzi huo, na Wademocrat wengi wana hofu kwamba Baraza la Seneti pia linaweza kunyakuliwa na kuwaona wapinzani wa Biden wakiwa wanadhibiti bunge katika muda wa miaka miwili ya mwisho ya muhula wake wa kwanza madarakani.

Cory Booker kutoka New Jersey, ameliambia shirika la Habari la ABC kuwa kwa kawaida chama kilichoko katika Ikulu ya Marekani hushindwa wakati wa uchaguzi wa bunge wa katikati ya muhula, lakini ukweli ni kwamba bado kuna njia imara za kufuata.

Hata hivyo, vyama vyote vya Democratic na Republican vimeelekeza nguvu zake katika jimbo la Pennsylvania, ambalo ni mojawapo ya majimbo yatakayotoa maamuzi kuhusu urari wa madaraka nchini Marekani.

Siku ya Jumatatu Biden anatarajiwa kufanya kampeni yake ya mwisho kabisa karibu na mji mkuu wa  Maryland, huku Trump akifanya kampeni katika jimbo la Ohio.

(AFP, AP)