1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden atangaza kuwania tena urais wa Marekani

Mohammed Khelef
25 Aprili 2023

Joe Biden ametangaza kuwania tena urais kwa kipindi cha pili, uamuzi ambao utawapima Wamarekani kama wako tayari kumkabidhi mzee wa miaka 80 miaka mingine minne ya uongozi, huku hasimu wake, Donald Trump, akimkosoa.

https://p.dw.com/p/4QXhO
USA, Accokeek | Präsident Joe Biden
Picha: Patrick Semansky/AP/picture alliance

Akitumia video fupi inayoanza na picha za tukio la Januari 6, 2021 wakati wa kuvamiwa kwa bunge la Marekani na wafuasi wa Trump, Biden alizinduwa kampeni zake siku ya Jumanne (Aprili 25) kwa ujumbe wa mshikamano dhidi ya kile anachokiita vita dhidi ya demokrasia ya Marekani.

"Nilipowania urais miaka minne iliyopita, nilisema tulikuwa kwenye vita kwa ajili ya roho ya Marekani na bado tumo kwenye vita hivyo. Suali linalotukabili ni ikiwa kwenye miaka ijayo, tutakuwa na uhuru zaidi ama kidogo, haki zaidi ama chache. Najuwa ninachotakuwa muwe, na nadhani nanyi pia munajuwa. Huu si wakati wa kuwa goigoi, ndio maana ninawania tena uraisi, kwa kuwa naijuwa Marekani." Alisema Biden.

Soma zaidi: Wabunge wa Marekani wauidhinisha ushindi wa Joe Biden

Kiongozi huyo alitangaza dhamira yake ya kuingia kwenye kinyang'anyiro cha urais kwa uchaguzi wa mwakani 2024 ili kutetea kiti ambacho miaka minne iliyopita alikitwaa kutoka mikononi mwa hasimu wake, Trump, ambaye naye alishatangaza kurudi tena ulingoni. 

Biden anayetokea chama cha Democrat aliyaelezea majukwaa ya chama cha upinzani cha Republican kama kitisho kwa uhuru wa Marekani, akiapa "kupambana dhidi ya kampeni yao ya kuweka ukomo wa huduma za afya kwa wanawake, kukata mfuko wa ustawi wa jamii na kupiga marufuku vitabu," akiwapachika jina la wafuasi wa siasa kali za MAGA, kifupisho cha Make America Great Again, yaani ifanye Marekani iwe tukufu tena, ambayo kaulimbiu ya Trump.

Trump amkosowa Biden

Kwenye taarifa yake mara tu baada ya Biden kutangaza nia ya kuwania tena urais, Trump alisema hata mtu anapowachukuwa marais watano waliofanya vibaya kabisa kwenye historia ya Marekani na kuwakusanya pamoja, basi hawawezi kufikia nusu ya madhara ambayo "Biden ameyasababisha kwa Marekani ndani ya kipindi cha utawala wake wa miaka minne." 

Indianapolis Jahreskongress der National Rifle Association (NRA)
Mgombea urais wa Marekani kupitia Republican, Donald Trump.Picha: EVELYN HOCKSTEIN/REUTERS

Miaka miwili baada ya kuchukuwa madaraka kutoka kwa Trump, Biden alifanikiwa kupata idhini ya Bunge kutoa mabilioni ya dola kukabiliana na janga la UVIKO-19 na ujenzi wa miundombinu mipya uliopelekea kupunguwa sana kwa ukosefu wa ajira, lakini ongezeko kubwa la gharama za maisha zimeifanya rikodi yake ya ukuwaji wa uchumi kupwaya.

Soma zaidi: Wafuasi wa Trump wavamia bunge, dunia yaduwaa

Chama chake cha Democrat kimeamuwa kucheza bahati nasibu ya kumrejesha tena kuwania wadhifa huo kutokana na umri wake wa miaka 80.

Kura za maoni zilizokusanywa na Reuters na Ipsos zinaonesha kuwa kiwango chake cha kukubalika kimesalia kwenye asilimia 39. 

Kamala Harris, makamu wake wa sasa wa rais, ndiye atakayekuwa pia mgombea mwenza wake kwa uchaguzi wa 2024.

Vyanzo: AP, Reuters