Wafuasi wa Trump wavamia bunge, dunia yaduwaa | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.01.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wafuasi wa Trump wavamia bunge, dunia yaduwaa

Viongozi wa dunia wameeleza kushtushwa na waandamanaji wenye vurugu waliovamia Bunge la Marekan kubadili matokeo ya uchaguzi wa rais wa Novemba 3 yaliompa ushindi Joe Biden. Uvamizi huo ulichochewa na rais Donald Trump.

Polisi katika eneo la Capitol walijibu maandamano hayo kwa kutumia bunduki na gesi ya kutoa machozi wakati mamia ya waandamanaji walipovamia na kutaka kulilaazimisha bunge kubatilisha ushindi wa Biden dhidi ya rais Donald Trump, muda mfupi baada ya Warepublican wenzake na Trump kuanzisha juhudi ya dakika za mwisho kutupilia mbali matokeo ushindi wa Biden.

Waziri mkuu wa Uingereza Borris Johnson katika ujumbe wa twitter alielezea matukio katika bunge la Congress kama fedheha, akisema Marekani ilisimamia demokrasia kote duniani na kwamba ilikuwa muhimu kwamba kunakuwa na mabadiliko ya amani ya uatwala.

Washington I Sturm gegen U.S. Capitol

Wafuasi wa Trump wakipigwa gesi ya kutoa machozi nje ya majengo ya bunge mjini Washington DC, Januari 6, 2021.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas alisema maadui wa demokrasia watatiwa hamasa na matukio ya vurugu katika eneo la Capitol, na kumtolea wito Trump kukubaliana na uamuzi wa raia.

Katika ujumbe wa Twitter uliochapishwa baada ya waandamanaji kuvamia makao makuu ya bunge la Marekani, Maas alisema vurugu zimesababishwa na matamshi ya uchochezi. "Trump na wafuasi wake wanapaswa kukubali maamuzi ya wapigakura wa Marekani an kuacha kuikanyaga demokrasia.

Mkuu wa polisi wa Washington DC Robert Contee amesema mtu mmoja alipigwa risasi katikati mwa maandamano hayo ya vurugu. Mwanamke huyi alikuwa katika hali mahututi baada ya kushambuliwa kifuani katika eneo la bunge, viliripoti vyombo vya habari nchini humo.

Contee alisema waandamanaji walitumia kemikali za kuwasha dhidi ya polisi na kulaazimisha kuingia bungeni, wafuasi wa rais Donald Trump. Contee amesema silaha zisizopungua tano zimekamatwa na watu wasiopungua 13 wametiwa mbaroni mpaka sasa.

Washington I Sturm gegen U.S. Capitol

Mfuasi wa Trump akipeperusha bendera yenye maneno yasema: Trump ndiye rais wangu.

Waandamanaji hao ambao wengi hawakuwa wamevaa barakoa, walivamia bunge mapema Jumatano, wakati wabunge wakikutana kuthibitisha ushindi wa raia mteule Joe Biden.

Wakati giza likiingia, maafisa wa usalama walikuwa wanatafuta njia kuelekea walipo waandamanaji hao, wakitumia magruneti ya moshi kujaribu kuwatawanya na kusafisha eneo karibu na bunge. Moshi mkubwa wa gesi ya kutoa machozi ulikuwa unaonekana. Meya wa DC Muried Bowser alitangaza amri ya kutotoka nje kuanzia saa 12 jioni.

Biden apata ushindi mwingine

Machafuko ya Capitol yamekuja siku moja baada ya Biden kupata ushindi mpya, ambapo chama chake cha Democratic kilitabiriwa ushindi katika uchaguzi wa marudio wa nafasi mbili za seneti jimboni Georgia, na hivyo kuwapa Wademocrat udhibiti kamili wa bunge.

USA Georgia Wahl | Jon Ossoff und Raphael Warnock

Washindi wa viti vya seneti katika jimbo la Georgia, Jon Ossoff na Raphael Warnock.

Kwa zaidi ya karne mbili, kikao hicho cha pamoja cha mabaraza ya bunge kimekuwa tukio la lisilotiliwa maanani sana la kuthibitisha mshindi wa urais -- lakini Trump aliwahimiza wanacama wa chama chake cha Republican kukataa matokeo.

"Rais wa Marekani anchochea mapinduzi. Hatutatishiwa. Hatutazuwiwa," Alitweet mwakilishi wa Democratic Karen Bass. Mwakilishi Val Demings pia alilaani uvamizi wa bunge kama ushahidi wa "mapinduzi yaliokuwa yakiendelea" -- katika maneno yaliorudiwa na nusu dazeni ya wabunge.

Wawakilishi Elaine Luria alisema aliondoka jengoni kwa sababu ya ripoti ya bomu la bombani na kusema aliamini aliskia milio ya risasi. "Sitambui nchi yetu hii leo na wabunge waliounga mkono machafuko haya hawastahili kuwawakilisha Wamarekani wenzao," alisema.

Washington I Sturm gegen U.S. Capitol

Rais Mteule Joe Biden akihutubia taifa kufuatia machafuko ya wafuasi wa Trump.

Biden na uhakika wa kuapishwa

Biden ana uhakika wa kuwa rais, huku Wademocrat wakidhibiti tayari baraza la wawakilishi, lakini zaidi ya Warepublican 140 wa baraza hilo, na dazen ya maseneta wa Republican wameungana na Trump katika kupinga matokeo hayo ingawa hakuna ushahidi wa udanganyifu uliyothibitishwa mahakamani.

Kiongozi wa maseneta wa Republican Mitch McConnell, mshirika wa karibu wa Trump katika kipindi chake chote cha urais, alikosoa pingamizi hilo katika hotuba ilioja hisia, akibainisha kwamba matokeo ya urais hayakuwa hata yanakaribiana.

"Wapigakura, mahakama na majimbo yamezungumza. Ikiwa tutabadili uamuzi wao, itaharibu jamhuri yetu milele," alisema McConnell, ambaye anatarajiwa kupoteza nafasi yake kama kiongozi wa walio wengi baada ya ushindi wa Wademocrat katika uchaguzi wa seneti jimboni Georgia.

Vikosi vya usalama vilifanikiwa kuwaondoa waandamanaji na kurejesha hali ya usalama kwenye majengo ya bunge, huku muda wa amri ya kuondoka kwenye mitaa ya Washington DC majira ya saa 12:30 jioni.

Chanzo: Mashirika