1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty yamtaka Biden kulifunga gereza la Guantanamo

8 Januari 2022

Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limemtaka Rais Joe Biden kuitimiza ahadi yake ya kulifunga gereza la Guantanamo wakati ambapo maadhimisho ya miaka 20 tangu kufunguliwa kwake yakiwa yanakaribia.

https://p.dw.com/p/45IGS
Protest gegen Folter
Picha: Tim Sloan/AFP/Getty Images

Gereza hilo lilifunguliwa mahsusi kwa ajili ya kuwazuia washukiwa wa ugaidi waliokamatwa na Marekani katika vita vyake dhidi ya ugaidi. Ni gereza lililo kwenye kambi ya jeshi la Marekani nchini Cuba na linajulikana kwa mbinu zake za kinyama za kuwahojis washukiwa ambapo wakosoaji wanasema zinajumuisha mateso.

"Kadri gereza hilo linavyozidi kutumika, ndivyo Marekani inavyozidi kutiliwa shaka kote duniani kuhusiana na masuala ya haki za binadamu," alisema Daphne Eviatar, mkurugenzi wa usalama katika mpango wa haki za binadamu kwenye shirika la Amnesty International.

USA Präsident Joe Biden
Rais Joe Biden wa MarekaniPicha: Saul Loeb/AFP

Aliyepanga mashambulizi ya Septemba 11 bado yuko Guantamano au Gitmo

Karibu watu 780 walizuiliwa katika gereza la Guantanamo au Gitmo tangu kufunguliwa kwake mnamo Januari 12, 2002, ambapo idadi yao kubwa hawajafunguliwa mashtaka yoyote.

Gereza hilo kwa sasa limesalia na wafungwa 39 akiwemo Khalid Shaikh Mohammed, mtu anayeshukiwa kupanga mashambulizi ya Septemba 11 huko Marekani.

Miongo kadhaa imepita sasa ila kesi ya Mohammed na wengine 4 bado iko katika hatua za awali kutokana na kucheleweshwa mara kadhaa. Wanatakiwa kukabiliwa na mashtaka ya kuhusika katika mashambulizi ya Septemba 11 katika mahakama ya kijeshi ila tarehe ya kesi hiyo bado haijawekwa.

"Guantanamo inatoa mfano mbaya sana kutokana na kuwa sheria hazifuatwi na pia kuna ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu kama mateso na watu kupotezwa," alisema Mathias Schreiber afisa wa Amnesty International alipokuwa akizungumza na shirika la habari la Ufaransa AFP.

Schreiber alitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuishinikiza Marekani kulifunga gereza hilo.

Kwanini gereza la Guantanamo bado liko wazi?

Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama aliamrisha gereza hilo lifungwe mwaka 2009 ila hilo halikufanyika kipindi cha utawala wake.

Mtangulizi wa Rais Biden Donald trump, alitaka gereza hilo liendelee kutumika ila Biden wakati wa kampeni, aliahidi kwamba atalifunga kabla muhula wake haujakamilika.

Chalid Scheich Mohammed Guantanamo Bay
Chalid Scheich Mohammed mmoja wa wafungwa wa GuantanamoPicha: Derek Poteet/AP/dpa/picture alliance

Bunge la Congress ndilo linalompinga Biden pakubwa kuchukua hatua ya kulifunga gereza hilo. Sheria bado inaifunga serikali ya shirikisho la Marekani kuwahamisha wafungwa wowote kutoka Guantanamo na kuwapeleka katika magereza ndani ya nchi ya Marekani.

"Ni msimamo wa muda mrefu wa White House ambapo vipengee vya sheria vinaizuia serikali kuamua ni lini na wapi itakapowafungulia mashtaka wafungwa waliozuiliwa katika gereza la Guantanamo na watakapopelekwa pindi watakapoachiwa," alisema Rais Biden katika taarifa.

Afisa wa shirika la Amnesty, Schreiber, alisema wafungwa wengi wanaweza kupelekwa katika nchi kama Ujerumani, ambayo tayari imewachukua wafungwa watatu wa Guantanamo na huenda ikawa tayari kuwachukua wafungwa zaidi.

Chanzo; https://bit.ly/3t8KUxx