1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aina mpya ya kirusi cha corona yaripotiwa Marekani

Sylvia Mwehozi
30 Desemba 2020

Aina mpya ya kirusi cha corona kinachoaminka kusambaa kwa kasi, imeripotiwa kwa mara ya kwanza nchini Marekani na Amerika ya Kusini wakati rais mteule wa Marekani Joe Biden akiapa kuzidisha juhudi za utoaji wa chanjo.

https://p.dw.com/p/3nLds
Symbolbild | USA | Coronavirus
Picha: Jeff Chiu/AP Photo/picture alliance

Aina hiyo mpya ya kirusi cha corona kilichogunduliwa kwa mara ya kwanza nchini Uingereza, sasa kimeripotiwa kuingia Marekani katika mji wa Colorado. Kirusi hicho kimegundulika kwa kijana wa miaka 20 ambaye hana historia ya kusafri. Taarifa za vyombo vya habari za ndani zinasema kuna uwezekano wa kisa kingine cha kirusi hicho. Wataalamu wanaamini kwamba aina hiyo mpya inaweza kuenea kwa kasi na itakuwa chanzo cha ongezeko la maambukizi Uingereza. Aina hiyo mpya ya kirusi kinachujulikana kama B.1.1.7 tayari pia imeripotiwa Canada, Italia, India na Umoja wa Falme za Kiarabu. Chile nayo imeripoti aina hiyo mpya na kulifanya kuwa taifa la kwanza Amerika ya Kusini kubaini maambukizi yake.

Rais mteule wa Marekani Joe Biden ameonya kwamba hali mbaya ya Covid-19 inaweza isiwe rahisi hadi kufikia mwezi Machi. Aidha Biden ameongeza kuwa changamoto iliyopo ni kampeni kubwa ya utoaji chanjo huko akiukosoa mpango wa mtangulizi wake Donald Trump katika usambazaji chanjo.

Österreich Impstart Senioren in Wien
Mfanyakazi wa afya Vienna baada ya kupewa chanjoPicha: Lisi Niesner/REUTERS

"Lakini kama nilivyohofia na kuonya kwa muda mrefu, juhudi za kusambaza na kutoa chanjo haziendelei kama inavyostahili. Wiki chache zilizopita, utawala wa Trump ulipendekeza kwamba Wamarekani milioni 20 wangeweza kupewa chanjo kufikia mwishoni mwa Desemba. Ikiwa hali itaendelea kama ilivyo sasa, itachukua miaka, sio miezi, kuwapatia chanjo raia wa Marekani" alisema Biden.

Shirika la afya la Umoja wa Ulaya ECDC lilionya Jumanne kuwa kuna hatari kubwa aina mpya ya kirusi cha Covid-19 inaweza kusababisha vifo zaidi na kuhatarisha huduma za afya kwa sababu ya "kuongezeka kwa maambukizi"

Wakati huohuo Amerika ya Kusini na Caribbean zimekuwa kanda ya pili baada ya Ulaya kufikia vifo nusu milioni vinavyotokana na covid-19 huku maambukizi yakipindukia milioni 15 katikati mwa msimu wa sikukuu. Zaidi ya theluthi moja ya vifo vimetokea Brazil. Juhudi za utoaji wa chanjo kwenye mataifa ya Argentina, Mexico, Chile na Costa Rica zimeleta matumaini kwa baadhi ya maeneo ya kanda hiyo.

Mataifa kadhaa yasitisha usafiri kutoka Uingereza kwa sababu ya aina mpya ya virusi vya corona

Serikali ya Uingereza imekuwa chini ya shinikizo la kuzidisha vizuizi wakati rekodi ya maambukizi mapya ikifikia 53,135 ndani ya saa 24. Ufaransa inakusudia kuanza marufuku ya usiku mapema jioni katika baadhi ya maeneo ya nchi. Waziri mwenye dhamana ya afya Olivier Veran, amesema hata hivyo serikali haitofunga shughuli za umma. Ufaransa hadi sasa imesajili visa milioni mbili na nusu na vifo nchini humo ni elfu 64,000.

Upande wa Asia, Thailand imetangaza hatua mpya, ikiwemo kufungwa kwa maeneo ya burudani wakati wa shereh za kuukaribisha mwaka mpya, katikati mwa ongezeko la maambukizi.