1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini inajipambanua kama mshirika muhimu kimataifa

Hawa Bihoga
27 Mei 2024

Afrika Kusini haibebi sifa ya kuwa taifa lililoendelea zaidi kiviwanda barani Afrika pekee, lakini inajijengea jina Kimataifa kama dola lenye nguvu kidiplomasia na kwa jumla kuwa sauti ya mataifa ya kusini mwa bara hilo.

https://p.dw.com/p/4gLau
Johannesburg, Afrika Kusini | Viongozi wa BRICS wakiwa katika picha ya pamoja.
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini akiwa akiwa katikati. Kutoka kushoto ni Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva, wa China Xi Jinping, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov.Picha: Prime Ministers Office/ZUMA Press/picture alliance

Afrika Kusini imekuwa mstari wa mbele katika kutatua migogoro kadhaa kwa njia ya amani barani Afrika, mfano, vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 2022 katika eneo la Tigray nchini Ethiopia.

Nje ya bara la Afrika, Afrika Kusini ilijaribu kuchukua nafasi kubwa ya upatanishi katika vita vya Urusi na Ukraine, Rais Cyril Ramaphosa alizungumza na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin na Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine na kusafiri hadi Kyiv na Moscow na ujumbe wa Afrika kwa mazungumzo mnamo Juni 2023.

Kama nchi pia imedumisha msimamo wake wa kutoegemea upande wowote.

Afrika Kusini na Urusi zimekuwa na uhusiano wa karibu tangu Vita Baridi, ambao umesababisha nchi hiyo mara kwa mara kutoshiriki kura nyingi za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, chaguo ambalo mataifa mengi ya Magharibi yanaona halieleweki.

Soma pia:Mahakama ya ICJ yaitaka Israel kusitisha mashambulizi huko Rafah

Taifa hilo la Kusini mwa Sahara lilizua taharuki wakati vita vinavyoendelea kati ya Israel na Hamas ikiishutumu Israel kwa mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza kwenye kesi iliyowasilishwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ mjini The Hague.

Hadi kufikia Mei 24 mwaka huu, ICJ, iliamuru "kusitishwa mara moja" kwa mashambulizi ya Israel katika eneo la Rafah, na hivyo kutekeleza ombi la dharura la Afrika Kusini.

Wachambuzi: Afrika Kusini ni mshirika muhimu kimataifa

Afrika- Urusi | Diplomasia | Rais Cyril Ramaphosa na Rais Vladimir Putin,
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini akiwa na mwenzake wa Urusi Vladimir PutinPicha: Mikhail Metzel/TASS/IMAGO

Steven Gruzd ambae ni mchambuzi na Mkurugenzi wa program na Utawala na Diplomasia Afrika katika Taasisi ya masuala ya Kimataifa Afrika Kusini, anakubali kuwa taifa hilo, ni mshirika muhimu kimataifa.

 " Afrika Kusini imetazamwa kwa namna tofauti namna ilivyowaunga mkono Wapalestina, lakini imekataa kuinyooshea kidole Urusi kutokana na namna ilivyokiuka Mkataba wa Kimataifa." Aliiambia DW Gruzd.

Kwa upande wake Lwazi Somya ambae ni meneja wa sera wa asasi ya kiraia ya Ofisi ya Uhusiano ya Kusini mwa Afrika, anasema, historia ya Afrika Kusini inaithibitishia kuwa na wajibu wa kipekee wa kimaadili kwa haki za binadamu na sheria za kimataifa.

Soma pia:Democratic Alliance yawataka Waafrika Kusini kuiangusha ANC

Pia Somya alikosoa ukosefu wa kutambuliwa kimataifa kwa kile alichokiita "msimamo wa kanuni."

Aidha kwa upande wake Gruzd anasema Afrika Kusini iliimarisha sera zake za kigeni ikilenga kuimarisha uhusiano wake na mataifa na kuongeza kuwa taasisi zake za kidemokrasia zimeiimarisha serikali.

Ushiriki wake kwenye jumuiya ya kimataifa

Hili linadhihirika haswa katika ushiriki wake mkubwa katika Umoja wa Afrika, vile vile ni nchi pekee ya Kiafrika katika G20 na mwanachama wa Kundi la mataifa yanayoinukia kiuchumi la BRICS.

Jumuiya hiyo, ambayo sasa inajumuisha nchi tisa zinazoshirikiana kiuchumi, sasa inadai sauti zaidi katika Umoja wa Mataifa, Shirika la Fedha la Kimataifa, Benki ya Dunia na Shirika la Biashara Duniani.

Kwanini Afrika Kusini inaishtaki Israel ICJ?

Taifa hilo pia linajaribu kuwakilisha maslahi ya mataifa yalio kusini mwa Afrika katika jumuia mbazo hazifungamani na siasa, mtandao wa mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yanajumuisha mataifa kama vile China, Brazil, India na Afrika Kusini yenyewe, shirika la Biashara Duniani na mashirika mengine ya biashara na maendeleo.

Soma pia:Pretoria yakaribisha ombi la ICC la kutaka kukamatwa kwa viongozi wa Israel na Hamas

Kwa mujibu wa Gruzd hili linaonesha kuwa Afrika Kusini imejidhatiti kufanyia mabadiliko miundo ya sasa ya mifumo ya kimataifa.

Kwa upande wake Sanusha Naidoo ambae ni mchambuzi katika taasisi ya Global Dialogue mjini Pretoria anaona kwamba Afrika Kusini na washirika wake wanatafuta "nafasi" katika muundo wa dunia uliopo kwa sasa ambapo ushirikiano thabiti unaweza kutumika kufanikisha hilo.