1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfrika Kusini

Democratic Alliance yawataka Waafrika Kusini kuiangusha ANC

27 Mei 2024

Chama kikuu cha upinzani Afrika Kusini Democratic Alliance kimetoa wito wake wa mwisho kwa wapiga kura kukisaidia kukiondoa madarakani chama tawala cha ANC wakati kilikamilisha kampeni zake kabla ya uchaguzi wa wiki hii.

https://p.dw.com/p/4gJF4
Kiongozi wa upinzani Afrika Kusini John Steenhuisen
Kiongozi wa DA John Steenhuisen anawarai wapiga kura wakiondoe madarakani chama tawala ANCPicha: MICHELE SPATARI/AFP

Akizungumza mbele ya maelfu ya wafuasi waliojitokeza jana katika eneo la Benoni, mashariki mwa Johannesburg, kiongozi wa chama hicho John Steenhuisen alisema kama wapiga kura wa Democratic Alliance watabaki majumbani, au waigawe kura miongozi mwa vyama vingi vidogo, basi sura ijayo ya nchi hiyo itakuwa mbaya hata zaidi kuliko siku za nyuma.

Soma pia: Vyama vya kisiasa nchini Afrika Kusini vimefanya kampeni katika wiki ya mwisho kabla ya uchaguzi mkuu

Democratic Alliance ndicho chama kikubwa kabisa nchini Afrika Kusini na kimekusanya baadhi ya vyama vidogo vya upinzani ili kuunda mkataba unaojulikana kama Mkataba wa Vyama vingi vya Siasa nchini Afrika Kusini, ambapo kundi la vyama vya kisiasa vitaziweka pamoja kura zao ili kukipinga chama tawala cha ANC baada ya uchaguzi. Uchunguzi wa maoni wa karibuni na wachambuzi wanadokeza kuwa ANC huenda kikapata chini ya asilimia 50 ya kura za kitaifa.

Democratic Alliance wako chini ya shinikizo baada ya ungwaji mkono wao kupungua katika uchaguzi uliopita wa kitaifa na viongozi wake kadhaa wakaondoka chama hicho ili kuunda vyama vipya vya kisiasa ambavyo vitashiriki katika uchaguzi huo. Uchaguzi mkuu wa Afrika Kusini utafanyika Jumanne wiki hii.