1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICJ yaiamuru Israel kusitisha mashambulizi Rafah

24 Mei 2024

Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ imeitaka Israel kusitisha mara moja mashambulizi yake huko Rafah, katika kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini kwa tuhuma kuwa vikosi vya Israel vinafanya mauaji ya halaiki huko Gaza.

https://p.dw.com/p/4gFvV
The Hague - Uholanzi | Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ
Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJPicha: Peter Dejong/AP Photo/picture alliance

Mahakama hiyo ya ICJ yenye makao yake mjini The Hague, Uholanzi imeiamuru Israel kusitisha operesheni za kijeshi huko Rafah, ukiwa ni uamuzi wa kihistoria ambao unaweza pia kuongeza shinikizo la kimataifa kwa serikali mjini Tel-Aviv baada ya zaidi ya miezi saba ya vita huko Gaza.

Majaji wa ICJ  wamesema Israel inapaswa kukomesha mara moja mashambulizi yake ya kijeshi, pamoja na hatua nyingine zozote katika mji wa Rafah, ambavyo vinaweza kuwasababishia Wapalestina huko Gaza kuishi katika hali ambayo wanaweza kukumbwa na madhila yanayoweza kuwa na athari za kimwili. Jaji Mkuu wa ICJ Nawaf Salam amesema:

" Mahakama inazingatia kuwa kwa wajibu wa sheria za Mkataba dhidi ya Mauaji ya Kimbari, Israel ni lazima isitishe mara moja mashambulizi yake ya kijeshi."

The Hague- Jumba la Ofisi za Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ
"Kasri la Amani"- Jumba la Ofisi za Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJPicha: Nikolai Sorokin/Zoonar/picture alliance

Aidha Mahakama hiyo kuu ya Umoja wa Mataifa imeiamuru pia Israel kukiwacha wazi kivuko cha Rafah ili kuhakikisha upatikanaji kamili wa misaada ya kibinadamu na kuwezesha ufikiaji wa kiwango cha huduma za msingi zinazohitajika haraka pamoja na usaidizi wa kibinadamu. Lakini pia ICJ imeamuru kuachiliwa kwa mateka wa Israel ambao bado wanashikiliwa na kundi la Hamas.

Hata hivyo  maamuzi ya ICJ huwa na umuhimu zaidi kisheria  lakini mahakama hiyo haina mifumo madhubuti ya kuyatekeleza moja kwa moja. Kwa mfano, iliiamuru Urusi isitishe uvamizi wake nchini Ukraine, bila mafanikio yoyote.     

Israel ambayo imekuwa ikitetea haki yake ya kujilinda imetoa hoja mbele ya mahakama hiyo kuwa uamuzi unaotaka usitishwaji wa operesheni za kijeshi, ungeliwanufaisha zaidi wanamgambo wa Hamas na kuwazuia wanajeshi wa Israel kuwaokoa watu waliochukuliwa mateka wakati wa shambulio la kikatili la kundi hilo mnamo Oktoba 7 mwaka jana.

Afrika Kusini yaupongeza uamuzi wa ICJ

Waziri Naledi Pandor (kulia) akiwa na mwenzake wa Ujerumani Annalena Baerbock
Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Naledi Pandor (kulia) akiwa na mwenzake wa Ujerumani Annalena BaerbockPicha: Thomas Koehler/photothek/picture-alliance

Afrika Kusini iliyowasilisha kesi hiyo imeupongeza uamuzi huo na kuzitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuunga mkono.  Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Naledi Pandor amesema anaamini kuwa uamuzi huu ni madhubuti zaidi katika hatua za muda na unatoa wito uliowazi wa kukomesha mashambulizi.

Soma pia: Afrika Kusini yaitaka ICJ kuishinikiza Israel kuhusu Gaza

Kwa upande wao maafisa wa Hamas wameumekaribisha mpango wa ICJ wa kutuma kamati ya uchunguzi huko Gaza na kuahidi kuwa watatoa ushirikiano.     

Hayo yanajiri wakati vita vikiendelea kupamba moto huko Gaza, huku juhudi za kidiplomasia zinazolenga  kufikiwa makubaliano ya usitishwaji mapigano zikiendelea.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anatarajiwa hivi leo kukutana kwa mazungumzo na mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa manne muhimu ya Kiarabu  ambayo ni Qatar, Misri Jordan na Saudi Arabaia na kujadili kuhusu vita huko Gaza kati ya Israel na kundi la Hamas.

(Vyanzo: Mashirika)