Afrika katika magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 25.10.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yamaendika juu ya mwito wa kuzifungua nyoyo za watu na mipaka ya bara la Ulaya kwa ajili ya wakimbizi. Pia yameandika juu ya mwito wa Askofu Mkuu wa Ujerumani Robert Zollitsch

Askofu Mkuu wa Ujerumani Robert Zollitsch

Askofu Mkuu wa Ujerumani Robert Zollitsch

Jarida la "Focus"limeandika makala yenye kichwa cha habari kinachosema "bakieni hapa, tunawahitaji." Gazeti hilo limemnukulu Kamishna wa Umoja wa Ulaya Kristalina Georgieva anaeshughulikia misaada ya kibinadamu akitoa mwito wa kuzifungua nyoyo na mipaka ya Ulaya kwa ajili ya wakimbizi. Jarida hilo pia limemkariri Askofu Mkuu wa Ujerumani Robert Zollitsch akisema kuwa bara la Ulaya halipaswi kujenga kuta ili kuwazuia wakimbizi kuingia.

Jarida la "Focus" linatufahamisha zaidi kuwa Kamishna wa Umoja wa Ulaya Kristalina Georgieva amelitaka bara la Ulaya liwe na moyo wa kutoa ili kuwasaidia wakimbizi.

Hatahivyo Jarida la "Focus" limemkariri mwanaharakati maarufu wa Ujerumani Rupert Neudeck akiarifu juu ya mpango wa kutoa mafunzo kwa vijana wa Mauritania ndani ya nchi hiyo chini ya kauli mbiu inayosema bora nafasi darasani kuliko nafasi ndani ya mashua ya hatari.

Wakimbizi wapigwa baridi Ujerumani

Wakati Kamishna wa Umoja wa Ulaya anatoa mwito wa kuwa na moyo wa imani , Gazeti la"Süddeustche" limeripoti juu ya maisha ya wakimbizi 30 kutoka Afrika katika mji wa Dachau uliopo katika jimbo la Bavaria kusini mwa Ujerumani.Gazeti hilo linatufahamisha kwamba wakimbizi 30 kutoka Afrika wamewekwa katika uwanja wa Tennis usiotumika tena. Usiku unapoingia baridi kali linazipenya kuta,umeme unakatika mara kwa mara na jiko ni dogo sana kwani lilijengwa ili kukidhi mahitaji ya kaya moja tu. Vitanda vya wakimbizi vimewekwa katika msafa na katika hali ya kubanana. Gazeti la "Süddeutsche" limemnukulu anaewajibika juu ya wakimbizi hao,Thomas Stanschus aliemo katika baraza la mji akisema kuwa hali inayowakabili wakimbizi hao ni kama ndoto mbaya.!

Afrika ipewe mafunzo ya upolisi

Gazeti la "Die Welt" limeripoti juu ya harakati za kupambana na ugaidi. Limemkariri mratibu wa harakati hizo wa Umoja wa Ulaya akitoa tahadhari.Katika mahojiano na gazeti hilo mratibu huyo Gilles de Kerchove ametoa mwito wa kutoa mafunzo kwa polisi wa Afrika. Mratibu huyo ameliambia gazeti la "Die Welt" kwamba Umoja wa Ulaya unapaswa kuchukua hatua thabiti,kwa mfano nchini Mali na Libya kwa lengo la kuzuia hatari.Ulaya inapaswa kutoa mafunzo ya polisi na ya kisheria katika nchi hizo, la sivyo itakabiliwa na changamoto nyingine katika siku za usoni.

Mratibu huyo wa harakati za kupambana na Ugaidi wa Umoja wa Ulaya Gilles de Kerchove ameliambia gazeti la "Die Welt" kwamba ikiwa Umoja wa Ulaya hautalisaidia zaidi bara la Afrika, basi litavamiwa na wakimbizi haramu, wahalifu,mihadarati na magaidi. Amesema watu wanapaswa kuanza kutambua kwamba bara la Afrika ni jirani wa karibu wa Ulaya.

Chuki dhidi ya mashoga Nigeria

Gazeti la "die tageszeitung wiki hii limeripoti juu ya chuki dhidi ya mashoga nchini Nigeria. Gazeti hilo limemkariri Waziri wa sheria Mohammed Adoke akiliambia baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa kwamba Nigeria haina haja ya mafunzo inapohusu ndoa za mashoga! Waziri huyo ameripotiwa na gazeti la "die tageszeitung" akisema kuwa ndoa za mashoga ni jambo linaloenda kinyume na utamaduni wa Nigeria.

Gazeti hilo limefahamisha kwamba mjadala juu ya mashoga nchini Nigeria unatokana na sheria iliyopitishwa mwishoni mwa mwezi wa Mei juu ya kuwafunga jela mashoga wote nchini Nigeria.Hata hivyo sheria hiyo bado haijatiwa saini.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri. Yusuf Saumu