Afghanistan yasitisha zoezi la kuwaachia wafungwa wa Taliban | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.08.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Afghanistan yasitisha zoezi la kuwaachia wafungwa wa Taliban

Serikali ya Afghanistan imesema kuwa haitowaachia huru wafungwa 320 waliobaki wa kundi la wanamgambo la Taliban, hadi pale kundi hilo litakapowaachia maafisa wa serikali.

Tangazo hilo kwa mara nyingine linayaweka rehani mazungumzo ya amani yaliyokuwa yamepangwa kuanza ndani ya siku chache zijazo. Mazungumzo hayo ya amani yalikuwa yaanze siku ya Alhamis wiki hii lakini sasa yameingia mashaka kutokana na tangazo hilo la serikali. Baraza la kitaifa la kijadi linalojulikana kama "Jirga", lilitaka kuachiwa mara moja wafungwa wa Taliban waliobaki na hivyo kufufua matumaini ya kuendelea na mchakato wa mazungumo.

Mkataba wa amani baina ya Marekani na Taliban ulilitaka kundi hilo kuwaachia maafisa 1,000 wa serikali na jeshi huku serikali ikiwawachia jumla ya wafungwa 5,000 iliyokuwa ikiwashikilia. Msemaji wa serikali ya Afghanistan Sediq Sediqqi amesema suala la kuwaachia wafungwa sio gumu ingawa kitendo hicho kinatakiwa kutekelezwa na pande zote mbili.

"Tumepokea wasiwasi kutoka kwa washirika wawili wa Afghanistan, Ufaransa na Australia. Afghanistan inashirikiana na nchi hizi mbili kuhakikisha hatua zipi zinafuata, katika kuangalia madai yao na wasiwasi. Lakini tena kama serikali tumesema mara nyingi kwamba hawa wafungwa 400 wa Taliban ni wahalifu .. Ni kitisho sio tu kwa usalama wa taifa la Afghanistan, lakini pia kwa usalama wa kitaifa wa washirika wetu ambao wamekuwa wakishirikiana nasi kwa muda mrefu, " aliongeza Sediqqi.

Kwa upande wake, msemaji wa Taliban Suhail Shaheen amesema kundi hilo limetimiza wajibu wake, na hawana taarifa ya afisa yeyote wa serikali ambaye bado anashikiliwa. Kundi hilo lilisema liko tayari kuanza mazungumzo na serikali ndani ya wiki moja mara baada ya zoezi la kuwaachia wafungwa litakapokamilika.

Afghanistan Kabul Taliban Freilassung

Baadhi ya wafungwa wa Taliban walioachiwa hivi karibuni

Mkataba wa amani na Taliban unalenga kukomesha vita ya Marekani nchini Afghanistan. Vikosi vya Marekani vilikuwa vimeanza kuondoka nchini humo na hadi kufikia Novemba wangekuwa wamesalia askari wasiozidi 5000 wa Marekani kutoka askari 13,000 waliokuwepo Afghanistan wakati makubaliano yanafikiwa mwishoni mwa Februari.

Chini ya makubaliano hayo, uondoaji wa majeshi ya Marekani hakutegemei kufanikiwa kwa mazungumzo ya ndani ya Afghanistan bali ahadi zilizowekwa na Taliban za kukabiliana na makundi ya kigaidi na kuhakikisha nchi hiyo haitumiwi kama msingi wa mashambulizi dhidi ya Marekani na washirika wake.

Tangu iliposaini makubaliano ya Februari, Taliban iliheshimu ahadi yake ya kutovishambulia vikosi vya Marekani na Jumuiya ya kujihami NATO, lakini imeendeleza mashambulizi dhidi ya vikosi va usalama vya nchi hiyo.

Serikali inataka usitishaji wa haraka wa mapigano wakati Taliban yenyewe ikisema masharti hayo lazima yakubaliwe kwenye mazungumzo. Ufaransa na Australia zinaunga mkono uamuzi wa serikali wa kutowaachia wafungwa waliobaki. Wakati huo huo Iran imekana madai yaliyotolewa na Marekani kwamba inashirikiana na kundi la Taliban. Kulingana na ripoti iliyotolewa na kituo cha utangazaji cha CNN, maafisa wa ujasusi wa Marekani wanadai kwamba Iran ilitoa marupurupu kwa wapiganaji wa Taliban ili wavilenge vikosi vya Marekani na washirika wake.

Vyanzo: Ap/Dpa