1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afghanistan yapiga kura kumchagua rais.

Lilian Mtono
28 Septemba 2019

Afghanistan wameanza kupiga kura kwenye uchaguzi wa rais wakati kukiwa na hofu itokanayo na kukosekana kwa maandalizi mazuri lakini pia mashambulizi yaliyopangwa kufanywa na wanamgambo wa Taliban.

https://p.dw.com/p/3QOdO
Präsidentschaftswahlen in Afghanistan 2019
Picha: DW/E. Mahdavi

Raia nchini Afghanistan wameanza kupiga kura mapema hii leo kwenye uchaguzi wa rais, katika wakati ambapo kuna wasiwasi kwamba idadi ya wapiga kura watakaojitokeza itaathiriwa pakubwa na kukosekana kwa maandalizi mazuri lakini pia mashambulizi yaliyopangwa kufanywa na wanamgambo wa Taliban.

Raia waliojitokeza kwenye vituo vya kupiga kura, pamoja na hofu hiyo ya mashambulizi lakini pia wameelezea wasiwasi wao na kuchoshwa na serikali iligubikwa na rushwa na kusambaa kwa machafuko kwenye vituo vya kupigia kura.

Katika mji mkuu, Kabul idadi ya waliojitokeza ilikuwa isiyotabirika na majira ya asubuhi ilikuwa ni nadra kuyaona makundi ya watu wakiwa kwenye vituo hivyo. Hakukutolewa idadi ya wapiga kura walioshiriki zoezi hilo mapema hii leo. 

Präsidentschaftswahlen in Afghanistan 2019
Raia walijitokeza mapema lakini baadhi ya vituo vilichelewa kufunguliwaPicha: DW/E. Mahdavi

Baadhi ya vituo havikuwa na wasimamizi hata baada ya baadhi yao kuwahi mapema na kusubiri kwa muda mrefu vituo hivyo kufunguliwa. Mmoja ya raia hao Imam Baksh, anayefanya kazi ya ulinzi amesema hakuwa na wasiwasi kuhusu usalama wake, wakati akisubiri kupiga kura, lakini alisema, hajui ampe nani kura yake. Akasema "Wote hawa hawana furaha na nchi yao".

Wagombea wakuu ni pamoja na rais anayekabiliwa na matatizo mengi Ashraf Ghani na mshirika wake wa serikali ya umoja iliyohudumu kwa miaka mitano, Abdullah Abdullah, ambaye tayari anamlalamikia mpinzani wake Ghani kwa kutumia vibaya mamlaka aliyonayo dhidi yake.

Afghanistan Kabul | Ashraf Ghani nach Gebet zum Opferfest
Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani (katikati) anakabiliwa na upinzani mkali na mpinzani wake Abdullah Abdullah. Picha: picture-alliance/AP Photo/N. Khan

Kumekuwepo na baadhi ya mashambulizi nchini humo.

Kwenye wilaya ya Sorkh Rod watu wawili wameuwawa na wengine 17 kujeruhiwa baada ya bomu kuripuka katika shule iliyotumika kama kituo cha kupigia kura, mjumbe wa halmashauri ya mkoa Sohrab Qaderi aliliambia shirika la habari la dpa.

Shambulio jengine lilitokea katika msikiti ambao pia ulikuwa kituo cha kupigia kura mjini Kandahar na kuwajeruhi watu wengine 14 akiwemo polisi mmoja, hii ikiwa ni kwa mujibu wa afisa wa polisi wa eneo hilo Mohammed Qasim Azad.

Uchaguzi wa mwisho wa urais nchini Afghanistan ulifanyika mwaka 2014, na ulikabiliwa na  madai makubwa ya rushwa yaliyochochea machafuko kiasi cha kusukuma Marekani kuingilia kati, kukabili machafuko hayo. Hakuna mshindi aliyetangazwa hatua iliyosababisha kuundwa kwa serikali ya umoja ambapo Ghani na Abdullah kushirikishana madaraka.

Taarifa ya Habari za Asubuhi - 28.09.2019

Katika hatua nyingine, tume huru ya uchaguzi nchini humo, IEC imesema haikuwa na mawasiliano na vituo 901 kati ya 4,942 kote nchini humo wakati uchaguzi ukiendelea. Mkuu wa IEC Hawa Alam Nuristani amesema akiwa mjini Kabul kwamba "tulituma vifaa kwenye vituo 4,942, lakini tumerejeshewa ripoti kwamba ni vituo 4,041 vilifunguliwa."

Afisa mwingine wa IEC amesema, hawakuwa na mawasiliano na vituo 901. Bado haikuwa dhahiri iwapo zoezi la kupiga kura lilifanyika kwenye vituo hivyo ama vililazimika kufungwa kutokana na shinikizo la Taliban.  

Kufuatia changamoto hizo, muda wa kupiga kura ukiongezwa kwa masaa mawili, hii ikiwa ni kulingana na afisa wa IEC, aliyekataa kutambulishwa. Hatua hii pia imechangiwa na baadhi ya maeneo kushindwa kuanza zoezi hilo katika muda muafaka.