WHO yatahadharisha juu ya ongezeko la corona wakati wa mashindano ya kandanda | Michezo | DW | 02.07.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

EURO 2020

WHO yatahadharisha juu ya ongezeko la corona wakati wa mashindano ya kandanda

Shirika la afya duniani WHO limetoa wito wa kuweka njia bora zaidi katika kufuatilia mashindano ya kandanda ya kugombea kombe la Ulaya wakati ambapo maambukizi ya corona yanaongezeka tena barani Ulaya.

WHO imesema mamia ya watu wamegunduliwa kuwa na maambukizi hayo, miongoni mwa watazamaji wa kandanda barani Ulaya kote. Mkuregenzi wa shirika la afya duniani kanda ya Ulaya Hans Kluge ametahadharisha juu ya hatari ya kuzuka wimbi jipya la maambukizi ikiwa nidhamu haitazingatiwa. Amesema maambukizi yaliongozeka kwa asilimia 10 wiki iliyopita kutokana na watu kukusanyika pamoja kwa wingi, kutokana na safari na kulegeza hatua za kudhibiti maambukizi.

Kluge amesema kitisho hicho cha kuongezeka maambukizi kinatokana na kuwepo aina mpya ya virusi vya corona kwa jina Delta vinavyosambaa kwa kasi tangu kubainika kwa mara ya kwanza nchini India.

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Ulaya Hans Kluge

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Ulaya Hans Kluge

Mkuregenzi wa shirika la afya duniani kanda ya Ulaya  Hans Kluge ameongeza kusema kuwa kutokana na idadi hiyo ya maambukizi, hakuna mahala ambako janga hilo limeondoka na kwamba yatakuwa makosa makubwa kwa raia na viongozi kufikiri kwamba janga hilo limetoweka. Amesema lengo lake sio kuwavurugia furaha mashabiki wa kandanda lakini anashauri kwamba kabla ya kusafiri kwenda kuwashangilia wachezaji wetu inatupasa sote tuwe waangalifu!

Mpaka sasa watu zaidi ya milioni 3.9 wameshakufa duniani kote kutokana na janga la corona. Mkurugenzi huyo wa shirika la afya duniani WHO kanda ya Ulaya Hans Kluge amesema inapasa kuwa na nidhamu la sivyo maambukizi yataongezeka zaidi.

Mchuano uliojaza mashabiki ni kati ya Ujerumani na Uingereza uliochezwa kwenye uwanja wa Wembley jijini London tarehe 29 Juni 2021.

Mchuano uliojaza mashabiki ni kati ya Ujerumani na Uingereza uliochezwa kwenye uwanja wa Wembley jijini London tarehe 29 Juni 2021.

Katika juhudi za kulinda afya, shirikisho la vyama vya kandanda barani Ulaya, UEFA limebatilisha tiketi zote walizouziwa watu nchini Uingereza kwa ajili ya mechi ya robo fainali kati ya England na Ukraine itakayochezwa mjini Rome mwishoni mwa wiki hii.

Urusi nayo imetoa taarifa kwa mara ya tatu juu ya kuongezeka kwa idadi kubwa ya vifo kutokana na maambukizi ya virusi vya corona, wakati nchini Uingereza maambukizi yanaongezeka licha ya zoezi  kabambe la kutoa chanjo. Mechi za nusu fainali na fainali za kombe la Ulaya zitachezwa nchini Uingereza wiki ijayo.

Chanzo:/AFP