1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 9 wauawa kwa risasi mjini Hanau, Ujerumani

Angela Mdungu
20 Februari 2020

Watu tisa wameuawa baada ya mtu mmoja kufyatua risasi katika maeneo mawili tofauti mjini Hanau katika jimbo la Hessen nchini Ujerumani jana Jumatano

https://p.dw.com/p/3Y2dd
Deutschland Hanau | Schießerei & Tote, Angriff auf Shisha-Bars
Picha: Getty Images/AFP/T. Lohnes

Mwendesha mashitaka wa serikali katika  eneo hilo amesema mapema leo kuwa mamlaka zinafanya uchunguzi kuhusiana na mauaji hayo yaliyofanywa katika baa mbili zinamovutwa shisha katikati mwa mji wa Hanau na kisha katika baa nyingine kwenye mji wa Kesselstadt.

Polisi nchini Ujerumani imesema mtuhumiwa wa mauaji hayo katika mji ulio magharibi mwa ujerumani wa Hanau alikutwa amekufa nyumbani kwake mapema leo. Polisi wa eneo hilo wamesema timu maalumu ya wataalamu ilikuta pia mwili wa mtu mwingine katika nyumba ya mtuhumiwa, lakini hakuna dalili ya mtu huyo kuhusika kwenye mauaji hayo. Hakuna majeruhi walioripotiwa kutokana na tukio hilo.

Siasa kali za mrengo wa kulia zahusishwa

Awali mtuhumiwa wa shamulio hilo anayehusishwa na siasa kali za mrengo wa kulia alituma video kwa njia ya  mtandao yenye urefu wa karibu saa moja akidai kuwa Ujerumani inaongozwa na taasisi ya siri yenye mamlaka makubwa. Katika vidio hiyo alitoa pia kauli dhidi ya wahamiaji kutoka nchi za Kiarabu na Uturuki.

Deutschland Hanau | Schießerei & Tote, Angriff auf Shisha-Bars
Uchunguzi ukiendelea eneo yalikofanyika mauaji katikati mwa mji wa HanauPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Probst

Miili ya watu waliouawa ilikutwa saa kadhaa baada ya milio ya risasi kusikika majira ya saa nne usiku. Taarifa ya msemaji wa ofisi ya mwendesha mashitaka wa eneo hilo inasema habari juu ya kuwepo kwa shambulio jingine la risasi katika mji jirani wa Lamboy hazijathibitishwa ingawa kulikuwa na ulinzi  mkali katika eneo hilo. Ulinzi zaidi umeimarishwa katikati mwa mji wa Hanau wenye takriani wakaazi 20, 000 na kwenye eneo la tukio.

Baada ya shambulio hilo msemaji wa serikali ya Ujerumani ameandika kupitia ukurasa wake wa tweeter kulaani tukio hilo na kutoa pole kwa wakazi wa eneo hilo. Naye meya wa mji huo Claus Kaminsky amesema  tukio hilo ni  baya na litasalia vichwani mwa wakaazi wa eneo hilo kwa muda mrefu.