1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 5,000 wameuawa Mariupol

Lilian Mtono
7 Aprili 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema jana kwamba Urusi inazuia uingizwaji wa misaada ya kiutu kwenye mji wa Mariupol kwa kuwa inataka kuficha ushahidi wa maelfu ya raia waliouawa katika mji huo.

https://p.dw.com/p/49ZKn
Ukraine Präsident Selenskyj in Butscha
Picha: Ronaldo Schemidt/AFP/Getty Images

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amekiambia kituo cha televisheni cha Habertuk cha nchini Uturuki kwamba Warusi wanaogopa kwamba hatimaye ulimwengu utaona kinachoendelea Mariupol, ingawa amesema hawatafanikiwa kuuficha ushahidi wote. 

Aidha amesema Moscow haiwezi kukwepa kuwajibika kutokana na idadi kubwa ya mauaji ya raia wa Ukraine waliouawa vitani.

Soma Zaidi:Zelenskiy alihutubia Baraza la Usalama, ataka Urusi iwajibishwe 

Amesema katika hotuba yake kupitia mtandao wa Telegram kwamba wanajua maelfu ya raia hawajulikani walipo, na kuongeza kwamba kuna machaguo mawili tu, kwamba huenda wameuawa au wamerejeshwa Urusi.

Meya wa mji uliozingirwa nchini Ukraine wa Mariupol amesema zaidi ya raia 5,000 wameuawa baada ya wanajeshi wa Urusi kuuzingira mji huo kwa kipindi cha mwezi mmoja. Meya huyo, Vadym Boichenko amesema jana kwamba miongoni mwao ni watoto 210.

Amesema wanajeshi wa Urusi walishambulia kwa mabomu majengo ya hospitali ikiwa ni pamoja na lile ambalo watu 50 waliungua na mto hadi kufa.

Ukraine Krieg | Zerstörung in Mariupol
Wakazi wa Mariupol wakiwa wanachota maji, katikati ya majengo yaliyoharibiwa na mashambulizi ya UrusiPicha: Alexander Ermochenko/REUTERS

Jeshi la Urusi limelizingira eneo la kimkakati la bandari ya Bahari ya Azov na kuzuia usambazwaji wa chakula, maji na nishati, pamoja na kulishambulia eneo hilo.

NATO yahofia Urusi kuendeleza vita kwa muda mrefu.

Katika hatua nyingine, katibu mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg amesema rais wa Urusi Vladimir Putin haonekani kuachana na matamanio yake ya kuidhibiti Ukraine na kuonya kwamba vita hivyo huenda vikaendelea kwa miezi ama hata mikaa kadhaa.

Stoltenberg ameongeza kwamba taarifa za kijasusi za NATO zinaashiria kwamba Urusi inajiandaa kwa mashambulizi makubwa zaidi mashariki mwa Ukraine, wakilenga kulikamata eneo zima la Donbas na kuweka daraja la nchi kavu la kati ya Urusi na Rasi ya Crimea.

Brüssel NATO-Generalsekretär Jens Stoltenberg
Katibu wa NATO, Jens Stoltenberg anahofia mashambulizi ya Urusi kuendelea kwa miaka.Picha: FRANCOIS WALSCHAERTS/AFP

Amewaambia waandishi wa habari mjini Brussels wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku mbili wa mawaziri wa mambo ya nje wa NATO kwamba jumuiya hiyo inahihitaji kuisaidia Ukraine, kuendeleza vikwazo na kuimarisha ulinzi.

Huku hayo yakiendelea, Marekani kwa upande wake imesema itaiwekea vikwazo vikali serikali ya Putin vitakavyoathiri mara moja uchumi wa taifa hilo kutokana na mauaji ya kiholela nchini Ukraine, ikiwa ni pamoja na yale ya mji wa Bucha. 

Soma Zaidi: Urusi yanyemelewa na vikwazo vingine vikali kutoka Magharibi

Vikwazo hivyo ni pamoja na kuzuia mali za watoto wa kike wa Putin, Mariya Vorontsova na Katerina Tikhonova lakini pia kuwazuia kwenye mfumo wa kifedha wa Marekani. Wengine watakaoguswa ni waziri mkuu wa Urusi, Mikhail Mishustin, mke na watoto wa waziri wa mambo ya nje Segey Lavrov pamoja na aliyewahi kuwa rais na waziri mkuu wa Urusi, Dmitry Medvedev.

Baadae leo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linataraji kupiga kura juu ya ama kuisimamisha Urusi kwenye baraza la haki za binaadamu la Umoja huo kufuatia madai ya mauaji iliyoyafanya nchini Ukraine. 

Tizama zaidi:

Ukraine yawahamisha kutoka mji wa Mariupol uliozingirwa

Mashirika: AFPE/APE