Wasyria waliokimbia mapigano Aleppo waanza kurejea
26 Januari 2026
Taarifa kutoka ndani ya Syria, zinasema watu wameanza kurejea makwao kwenye mji wa Aleppo hususani baada ya serikali kutangaza kurefusha muda wa kusitisha mapigano kati ya vikosi vyake na wapiganaji wa Kikurdi wa SDF wanaoungwa mkono na Marekani.
Tangazo la kurefushwa muda kati ya pande hizo mbili limelotolewa na serikali mjini Damascus jana Jumapili. Maelfu ya watu waliukimbia mji wa Aleppo mapema mwezi huu kukwepa mapambano makali yaliyozuka kati ya vikosi vya serikali na SDF.
Wengi walikimbilia kwenye miji miwili jirani ambayo ilifurika watu na kusababisha ukosefu mkubwa wa mahitaji muhimu. Miongoni mwa miji hiyo ni ule wa Kobane ambao una idadi kubwa ya jamii ya wachache nchini Syria ya Wakurdi.
Vikosi vya serikali viliingia kwenye miji hiyo siku ya Jumamosi baada ya wapiganaji wa SDF kuyaachia maeneo makubwa ya ardhi kwa hiyari wakisema ni kwa lengo la kuepusha umwagaji damu.
Msongamano wa watu hasa kwenye mji wa Kobane ulizusha miito ya kutumwa misaada ya kiutu na serikali ya Syria ilitangaza jana Jumapili kufungua njia kwa mashirika ya kimataifa kupeleka misaada. Umoja wa Mataifa umesema tayari msafara wenye mahitaji muhimu umewasili Kobane.
Umoja wa Mataifa wapeleka vyakula na mafuta mji wa Kobane
Mapema wiki iliyopita, wakaazi wa mji huo waliliambia shirika la habari la AFP kwamba hawana chakula cha kutosha, maji wala umeme na wimbi la watu wanaokimbia mapigano lilikuwa linaongezeka.
Shirika la misaada ya kiutu la Umoja wa Mataifa - OCHA, limeiambia AFP kwamba malori 24 yaliyobeba "msaada wa kuokoa maisha, ikiwemo mafuta, mikate na vyakula vilivyo tayari kuliwa" imewasili Kobane. Serikali imesema imefungua njia nyingine kuelekea mji mwingine jirani wa Hasakeh ambao nao umeshuhudia wimbi la waliokimbia mapigano.
Mji huo unaofahamika pia kwa kiarabu kama Ain al-Arab ulikuwa alama ya ushindi kwa wapiganaji wa Kikurdi zaidi ya miaka kumi iliyopita wakati walipokuwa wakipigana dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS.
IS ilifanikiwa kukamata eneo kubwa la ardhi ya Syria na Iraq katikati mwaka 2014 na kutangaza kile ilichokiita dola inayofuata sheria za kiislamu.Mwaka 2015 kwa msaada wa Marekani wapiganaji wa Kikurdi waliukomboa mji wa Kobane kutoka mikononi mwa IS.
Hata hivyo mnamo wiki za karibuni, utawala mpya nchini Syria umeendesha kampeni kubwa ya kijeshi kuchukua udhibiti wa maeneo makubwa upande wa kaskazini ambayo yamekuwa chini ya wapiganaji wa Kikurdi kwa zaidi ya miaka 10.
Serikali inataka kundi la SDF liweke chini silaha na wapiganaji wake wajumuishwe kwenye vikosi vya taifa huku ikiahidi kulinda haki za jamii ya Wakurdi ambao kwa miongo chungunzima wanalalamika kuonewa ndani ya Syria, nchini Iraq pamoja na Uturuki.