1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wasemavyo wahariri wa Ujerumani Alhamisi

Admin.WagnerD21 Aprili 2016

Alhamisi (21.04.2016) Wahariri wa Ujerumani wanaangazia maadhimisho ya miaka 90 ya kuzaliwa kwa Malikia Elizabeth, uchaguzi wa mchujo nchini Marekani na uamuzi wa mahakama Ujerumani kuhusu sheria ya ugaidi.

https://p.dw.com/p/1IaT9
MAjaji wa mahakama ya Katiba ya Ujerumani wamesema sheria ya ugaidi inakiuka haki za msingi za raia.
MAjaji wa mahakama ya Katiba ya Ujerumani wamesema sheria ya ugaidi inakiuka haki za msingi za raia.Picha: picture-alliance/dpa/U. Deck

Mhariri wa gazeti la Volksstimme juu ya mkutano kati ya mabalozi wa jumuiya ya NATO na Urusi uliofanyika jana mjini Brussels. Mhariri huyo anasema mdahalo kati ya NATO na Urusi ulivunjika mwaka 2014, kufuatia hatua ya Urusi kuliteka jimbo la Crimea kutoka Ukraine. Kufikia sasa misimamo ya pande hizo mbili iko mbali kabisa, na inaonekana itakuwa hivyo kwa muda mrefu, maadamu Urusi inaendelea kuikalia kinyumbe na sheria rasi hiyo ya Crimeria

Kuhusu sheria ya Ugaidi nchini Ujerumani BKA

Mahakama ya katiba nchini Ujerumani imetoa uamuzi kwamba baadhi ya vipengele vya sheria inayokipa kitengo cha polisi ya jinai BKA, mamlaka ya kufanya uchunguzi wa kupambana na ugaidi vinakwenda kinyume na katiba. Juu ya hukumu hiyo, mhariri wa gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger ameandika:

Laiti ukiukaji wa haki za msingi ungelikuwa kosa la jinai, basi ingelikuwa bayana sasa, baada ya uamuzi huo, kwamba bunge la Ujerumani linafanya mfululizo wa makosa. Katika kipindi cha zaidi ya miaka 15 tangu kutokea kwa mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11 nchini Marekani, mahakama ya katiba imesema bunge hilo limekuwa likipuuza haki ya faragha katika maamuzi yake. Hukumu ya BKA ni ya kihistoria kwa sababu inadhibiti matumizi ya nyenzo zote za kupambana na ugaidi n.k kikatiba.

Wahariri wanasema mchakato wa kura za mchujo umeonyesha mgawiko mkubwa zaidi miongoni mwa Wamarekani.
Wahariri wanasema mchakato wa kura za mchujo umeonyesha mgawiko mkubwa zaidi miongoni mwa Wamarekani.

Mchakato wa kutafuta wagombea wa urais Marekani

Mhariri wa gazeti na Münchner Merkus ameandika juu ya mchakato wa kura za mchujo unaoendelea nchini Marekani, kuelekea uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka huu. Mhariri huyo anasema:

Muda mfupi kabla ya kumalizika kwa mchakato wa kura za mchujo, inaonekana kana kwamba mfumo wa kiimla wa vyama viwili unaelekea kuvunjika na kuwa wa vyama vinne. Kwa Wademokrat na Warepublican pia, hali ya kutoridhika miongoni mwa wapigakura inadhihirika wazi. Rais Barack Obama aliingia madarakani miaka minane iliyopita ili kuondoa mfumo huo na mgawanyiko miongoni mwa Wamarekani. Lakini kwa jinsi mambo yanavyoonekana, ndoto yake imesambaratika. Hili ni chungu kwake, lakini ni chungu zaidi kwa Marekani.

Miaka 90 ya kuzaliwa Malkia Elizabeth II

Mhariri wa gazeti la Westfälischen Nachrichten ameandika juu ya Malkia wa Uingereza Elizabeth wa pili ambaye siku ya leo ametimiza miaka 90 ya kuzaliwa. Mhariri huyo anasema:

Kwa Waingereza wengi Malkia Elizabeth ndiye mhimili wa utulivu katika ulimwengu uliojaa misukosuko, vitisho na migogoro ya kisiasa na kiuchumi. Ni wachache sana wanaowazia kung'atuka kwake kwenye kiti cha umalkia, na kwa nini wawazie hilo? Hata Malkia mwenyewe hana mawazo hayo, anajiona kikazi zaidi hata katika umri wa miaka 90, baada ya kuongoza kwa miaka mingi zaidi kuliko watangulizi wake wote.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Gakuba Daniel