Wanaotaka kujitenga wajaribu tena kumrejesha Puigdemont | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.05.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Wanaotaka kujitenga wajaribu tena kumrejesha Puigdemont

Wanaotaka kujitenga jimboni Catalonia, wamekutana mjini Berlin na kuapa siku ya Jumamosi kufanya jaribio jingine tena kumrejesha  madarakani kiongozi wao aliyeko uhamishoni Puigdemont na kwamba hawataki uchaguzi mpya.

"Hatutaki uchaguzi  mpya," amesema  Eduard Puyol, msemaji  wa kundi linalomuunga  mkono Pigdemont  la  Together for Catalonia, pamoja  kwa  Catalonia.

Spanien Barcelona Demonstration für inhaftierte katalanische Politiker (Getty Images/AFP/J. Lago)

Mwanamke mmoja akishikilia bango linalosema Puigdemont rais wa jamhuri ya Catalonia

Hata  hivyo  juhudi kama  hizo  zitafanywa  kumrejesha  madarakani rais  wa  zamani  wa  Catalonia  ifikapo  Mei 14 aliongeza  Puyol baada  ya  mazungumzo  na  Puigdemont  mjini  Berlin.

Puigdemont aliondolewa  madarakani  na  serikali  kuu  mjini  Madrid baada  ya  Catalonia  kutoa  tamko  linalotangaza  uhuru  wa  jimbo hilo  mwaka  jana  kufuatia  kura  ya  maoni  iliyofanyika  katika jimbo  hilo ambayo  haikuidhinishwa  na  serikali  ya  Uhispania.

Kiongozi  huyo  wa  uhuru  wa  jimbo  la  Catalonia baadaye aliondoka  na  kwenda uhamishoni nchini  Ubelgiji. Juhudi  za  hapo kabla  za  kutaka  kumrejesha  madarakani  zilizuiliwa  na  mahakama ya  Uhispania.

Puigdemont alikamatwa  nchini  Ujerumani Machi  mwaka  huu baada  ya  Uhispania  kutoa  waranti wa  kukamatwa  kwake  barani Ulaya. Baadaye  aliachiliwa  kwa  dhamana.

Siku  ya  Ijumaa  bunge  la  Catalonia  linalounga  mkono  uhuru  wa jimbo  hilo liliunga  mkono  sheria  inayoruhusu  kurejeshwa  kwake madarakani  wakati  akiwa  nje  ya  nchi, kitu  ambacho  serikali  ya Uhispania imekataa.

Deutschland Puigdemont - Berlin (picture-alliance/dpa/B. Pedersen)

Rais wa zamani wa jimbo la Catalonia nchini Uhispania Carles Piugdemont baada ya mkutano na wabunge wa bunge la Catalonia mjini Berlin

Rais Halali

Ines Arrimadas, kiongozi  jimboni  Catalonia  wa  chama kinachopinga  uhuru  Ciudadamos Party, ameikataa sheria  hiyo aliyoiita  ya  "Puigdemont", akiieleza  kuwa "imetengenezwa  kwa ajili  ya  mkimbizi".

Tangu  alipoikimbia  Uhispania  Puigdemont  amekuwa  mtu anayesababisha  mgawanyiko  miongoni  mwa  wanaotaka kujitenga.

Siku  ya  Jumamosi kundi lenye ushawishi  mashinani  linalounga mkono  uhuru  la  ANC lilitangaza  matokeo  ya uchunguzi  wa  maoni, likisema  kwamba  wengi  wa  wanachama  wake  wanaunga  mkono kurejea  kwa  "rais halali".

Hata  hivyo , iwapo  hilo  litashindikana, waungaji  mkono  wa  ANC wanataka  serikali  mpya  iundwe  bila  ya  kurejea  katika  upingaji kura.

Bunge  la  jimbo  hilo linapaswa  kuchagua  rais  mpya  ifikapo  Mei 22 ama itayarishe  uchaguzi  mpya.

Deutschland Treffen von Junts per Catalunya in Berlin (picture alliance/dpa/G. Fischer)

Carles Puigdemont rais wa zamani wa jimbo la Catalonia katika mazungumzo na wabunge wa jimbo hilo mjini Berlin

Iwapo Puigdemont  hatarejeshwa  madarakani, waungaji  wake mkono  watapendekeza  kwamba  kiongozi  wa  ANC Jordi Sanchez, ambaye  kwa  sasa  yuko  kifungoni  mjini  Madrid  kuhusiana  na juhudi  za  kudai  uhuru  kushindwa, apewe  kazi  hiyo.

Lakini  mwezi  uliopita  mahakama  kuu  ya  Uhispania  ilikataa  ombi la  Sanchez  kutolewa  kutoka  jela  na  kuapishwa  kama  kiongozi wa  jimbo  hilo.

Iwapo hatua  hiyo itashindikana  "tutafungua  mlango  wa uwezekano mwingine," Pujol aliwaambia  waandishi  habari  mjini  Berlin, na kuongeza  kwamba "hakuna  jina  mlilotabiri  ambalo  linajadiliwa". Vyombo  vya  habari vya  Uhispania  vilitaja  jina  la mtaalamu  wa uchumi Elsa Artadi, ambaye  ni  mshirika  wa  Puigdemont.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Caro Robi

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com