Wairan waliokimbia nchi waanza kurejea nyumbani
16 Januari 2026
Mamia ya Wairani walionekana siku ya Ijumaa wakirejea nchini mwao wakitokea Uturuki kupitia mpaka wa nchi hizo mbili, wakati mashirika ya haki za binaadamu na raia wakisema msako mkali uliofanywa na vyombo vya dola umefanikiwa kuyasimamisha maandamano kwa sasa.
Akizungumza akiwa kwenye mpaka wa Kapikoy uliopo kwenye jimbo la mashariki mwa Uturuki la Van, Isa Velizadeh, amesema haoni tena sababu ya kubakia Uturuki kwa kuwa hali nchini mwake imeshatulia:
"Ndiyo, niliingia Uturuki siku tatu zilizopita. Mashaka yalishapunguwa kwa kiasi fulani tangu juzi. Kwa siku hizi tatu hatujapata habari kutoka huko, lakini kwa kile tunachokiona kwenye televisheni za Uturuki ni kwamba mambo yamepowa kwa sasa," amesema Isa Velizadeh.
Licha ya ugumu wa mawasiliano ya intaneti ndani ya Iran kwenyewe, wakaazi kadhaa waliopata fursa ya kuzungumza na shirika la habari la AFP siku ya Ijumaa wamesema hali kwenye mji mkuu, Tehran, imekuwa tulivu tangu Jumapili. Wakaazi hao wanasema droni zimekuwa zikiruka juu ya anga ya Tehran, ingawa hakuonekani ishara yoyote ya maandamano mapya.
Putin azungumza na Netanyahu kuhusu matukio ya Iran
Kwa upande mwengine, Rais Vladimir Putin wa Urusi alizungumza kwa njia ya simu siku ya Ijumaa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na Rais Masoud Pezeshkian wa Iran, katika jitihada za kuzuwia athari za maandamano ya Iran kugeuka kuwa vita kamili kati ya pande hizo mbili.
Msemaji wa Ikulu ya Urusi, Dmitry Peskov, amesema hali kwenye eneo la Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati imezidi kuwa tete, na kwamba Rais Putin amewaambia viongozi hao wawili kwamba yuko tayari kuwa mpatanishi wao.
Moscow ni mshirika wa karibu wa Iran na ina mahusiano mazuri na Israel, licha ya ukosoaji wake mkubwa dhidi ya Netanyahu kwa matendo ya Israel katika Ukanda wa Gaza tangu Oktoba 7, 2023.
Hii ni mara ya pili kwa Urusi kupendekeza kuwa mpatanishi kati ya Israel na Iran katika miezi ya hivi karibuni, mara ya mwisho ukiwa wakati wa vita vya siku 12 vilivyotokana na uchokozi wa Israel dhidi ya Iran, ambavyo baadaye Marekani ilijiunga navyo kwa kuvishambulia vinu vya nyuklia vya jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Iran inazishutumu Israel na Marekani kwa kuchochea maandamano na machafuko ya hivi karibuni, ambayo wanaharakati wanadai yaliangamiza maisha ya zaidi ya watu 3,000. Marekani ilitishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran ikiwa itawakandamiza waandamanaji.
Tehran inasema Tel Aviv na Washington zilitarajia kutumia machafuko hayo kuiangusha serikali na kuligawa taifa hilo la Ghuba, kwa mtindo ule ule ambao umefanyika kwenye mataifa mengine ya Kiislamu na Kiarabu, zikiwemo Libya, Iraq, Afghanistan, Syria na Yemen.