1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wagombea wa Democratic wachuana kwenye mdahalo mwingine

20 Desemba 2019

Wanasiasa wanaowania kuteuliwa kugombea urais kupitia chama cha Democratic katika uchaguzi mkuu wa mwakani nchini Marekani wamechuana usiku wa kuamkia leo kwenye mdahalo wa mwisho kwa mwaka 2019.

https://p.dw.com/p/3V83q
USA: TV-Debatte der Demokraten
Wagombea wa Democratic wakiwa kwenye mdahalo wa Alhamisi usiku.Picha: Reuters/M. Blake

Mdahalo huo ulijumuisha mashambilizi dhidi ya Rais Donald Trump na makabiliano miongoni mwao wenyewe. 

Siku moja tangu Baraza la Wawakilishi kupiga kura ya kumfungulia mashtaka Rais Trump, wagombea saba wa Democrat wameungana na kusisiitza ulazima wa kumshinda rais huyo wa 45 wa Marekani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Wakati wa mdahalo wa usiku wa kuamkia leo, mwanasiasa anayepewa nafasi ya kuteuliwa na chama cha Democrat, Joe Biden, amesema wana wajibu wa kurejesha heshima ya kiti cha urais kwa kuwa Trump ameidhoofisha kwa kiwango ambacho hakikutarajiwa.

Seneta Bernie Sanders ambaye kura za maoni ya umma zinamuweka katika nafasi ya pili katika mchuano wa Democratic, alimshambulia Rais Trump kwa kuongoza kile alichookiita kuwa "utawala uliojaa rushwa katika historia ya nchi hiyo."

Mwanasiasa mwingine, Elizabeth Warren, amesema Trump anapuuza watu masikini na kuendekeza rushwa.

"Nionavyo mimi, sasa tumeshuhudia madhara ya rushwa. Na kilicho  wazi kwenye kinyang'anyiro cha mwaka 2020, ni kwa jinsi gani tutapambana dhidi ya rais mpenda rushwa kuliko wote katika historia." alisema wWarren.

Trump aushambulia mdahalo huo

USA: TV-Debatte der Demokraten
Seneta Elizabeth Warren na Meya pete ButtigiegPicha: AFP/F. J. Brown

Timu ya kampeni ya Rais Trump iliushambulia mdahalo huo wa jana kwa kuutaja kuwa uliokosa nuru na usio na matumaini na kuongeza ndiyo sababu chama cha Democrat kinataka kumuondoa madarakani rais huyo kwa kuwa hakina mgombea mwenye vigezo.

Baada ya miito ya kutaka kurejeshwa kwa misingi ya maadili katika ikulu ya White House, mdahalo uligeukia masuala mengine mengi ikiwemo sera za biashara, afya na jinsi ya kupambana na umasikini - masuala ambayo yalizusha mnyukano miongoni mwa wagombea.

Senata Elizabeth Warren alianzisha mashambulizi makali dhidi ya mgombea hasimu, Pete Buttigieg, akisema meya huyo wa mji wa South Bend, Indiana, amekuwa akifanya vikao vya siri vya kuchangisha fedha kutoka kwa mabilionea ikiwemo kikao kilichofanyika kwenye jumba la kificho la tajiri mmoja huko California.

Buttigieg, ambaye nafasi yake katika kinyang'anyiro hicho imeimarika miezi michache iliyopita, aliyapinga madai hayo na kisha kumshambulia Warren kwa kuwa na utajiri mkubwa ambao ni karibu mara mia 100 ya kiwango cha fedha ambacho Buttegieg anafahamika kuwa nacho.

Mdahalo huo ni wa mwisho mwaka 2019 

USA: TV-Debatte der Demokraten
Picha: AFP/R. Beck

Wagombea wanaopewa nafasi ya kuteuliwa, wakiwemo Seneta Amy Klobuchar, bilionea Tom Steyer na mjasiriamali Andrew Yang, walijikita zaidi katika kuondoa wasiwasi kwa wapiga kura wanaofadhaishwa na siasa za Marekani.

Makamu wa rais wa zamani, Joe Biden, aliye mashuhuri miongoni mwa jamii za wafanyakazi na Wamarekani weusi, ameahdii kuirejesha Marekani kama ilivyokuwa chini ya utawala wa Barack Obama na kuokoa kutoka siasa za migawanyiko chini ya Trump.

Mdahalo huo, ambao ni wa mwisho kwa mwaka 2019, uliwajumuisha wagombea saba pekee kati ya 15  wanaowania kuteuliwa na chama cha  Democrat na umefanyika wiki sita kabla ya kufanyika kura ya kwanza ya mchujo huko Iowa mwezi Februari 2020.