Wagombea Tanzania walalamikia uhalifu kwenye kampeni | Matukio ya Afrika | DW | 24.09.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Wagombea Tanzania walalamikia uhalifu kwenye kampeni

Wakati zoezi la kampeni za uchaguzi mkuu likiendelea Tanzania baadhi ya vyama vya siasa vimesema vimeshuhudia baadhi ya mabango na picha zao kuchafuliwa huku baadhi ya maeneo vikilalamikia bendera zao kushushwa

Matukio hayo ni kinyume na maadili ya uchaguzi ya 2020. Vyama hivyo ni vile ambavyo vinashuhudiwa kuwa na mchuano mkali kwenye majukwaa ya kisiasa katika kunadi sera zao kwa wananchi, vinasema katika baadhi ya majimbo na kata kadhaa wagombea wao wamelalamika kuhujumiwa kwa picha na mabango zinazonadi sera zao jambo ambalo linakwenda kinyume na maadili.

Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano na Umma, Chama Cha Wananchi CUF, Abdul Kambaya amesema, katika baadhi ya majimbo wameshuhudia bendera za vyama vyao zikishushwa baada ya kuzipandisha, hatua ambayo wanaona huenda ikahatarisha amani katika kipindi hiki ambacho taifa ikielekea katika zoezi muhimu la kidemokrasia na kikatiba.

Tansania Anhänger der Oppositionspartei (CUF) während der Veranstaltung zur Begrüßung ihres Vorsitzenden Prof. Ibrahim Lipumba

Wafuasi wa chama cha CUF

Kadhia kama hiyo pia imeshuhudiwa kwa baadhi ya wagombea wa chama tawala CCM hasa katika maeneo ambao yameonekana kuwa na ushindani mkubwa wa kisiasa ikiwemo katika jiji la Dar es Salaam, ambapo mwenyekiti wa jumuia ya vijana taifa, Heri James anasema hadi sasa jimbo la Kawe picha za mgombea ubunge kupitia chama chake Askofu Joseph Gwajima zimeondolewa katika baadhi ya maeneo.

Wakati vyama hivyo vikiendelea kushuhudia vitendo vya kuashiria uvunjifu wa maadili ya uchaguzi baadhi ya vyama vya siasa vimekuwa vikitumia majukwaa ya kisasa mbali na kunadi sera zao, kuwasihi pia wanachama na wafuasi wao kuhakikisha hawaingilii mikutano ya vyama vingine, kutohujumu mabango, picha na vipeperushi vya wagombea wengine, wala matangazo ya Tume ya Uchaguzi. Hassan Almas ni katibu mkuu wa chama cha NRA

Maadili ya uchaguzi yaliyoridhiwa na wadau wa uchaguzi mapema mwaka huu, yameonya vikali kwa wananchama na wafuasi wa vyama vya siasa kuhakikisha wanaheshimu mabango na picha za wagombea wa vyama vingine. Mkurugenzi wa huduma za sheria kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi Emanuel Kawishe amesema hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika kuhujumu picha kwani jambo hilo linaweza kuvuruga amani. Uchaguzi mkuu nchini Tanzania umepangwa kufanyika Oktoba 28. 

Mwandishi: Hawa Bohoga DW, Dar es Salaam